Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa ya Tanzania bara yenye fursa nyingi sana za uwekezaji. Aidha, jiografia ya Mkoa wa Kigoma inaufanya kuwa Mkoa wa kimkakati katika kuvutia uwekezaji na maendeleo ya biashara za ndani na za kimataifa kutokana na kupakana na Nchi jirani za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia. Mkoa umezungukwa na Ziwa Tanganyika pia unaunganishwa na Mikoa ya Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es salaam kwa Reli ya Kati. Ziwa Tanganyika na Reli ya Kati ni fursa ya usafirishaji rahisi na nafuu wa bidhaa, malighafi na watu. Aidha, jiografia ya Mkoa pamoja na miundombinu iliyopo ni kuchochea cha maendeleo ya viwanda na biashara kutoka ndani na nje ya Mkoa na Nchi za Maziwa Makuu.