Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa ya Tanzania Bara yenye ardhi yenye rutuba ya kutosha, uoto wa asili na hali ya hewa ya kuvutia. Mkoa pia unayo bionuai adimu yenye kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi. Ipo milima, mabonde, Mito na Ziwa Tanganyika ambalo linashika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na kina kirefu cha maji. Kwa ujumla jiografia ya Mkoa wa Kigoma inaufanya kuwa Mkoa wa kimkakati kwa uwekezaji wa kitalii, kilimo, Viwanda na biashara. Aidha, shughuli za kiuchumi katika Mkoa zimeendelea kuimarika kutokana na jitihada za Serikali za kuboresha huduma mbalimbali za kijamii, miundombinu ya barabara, Reli, umeme na usafiri wa anga.
CHIMBUKO / ASILI YA MKOA.
MAENEO YA UTAWALA
Kwa upande wa maeneo ya Utawala, Mkoa umeendelea kukua kwa kasi nzuri. Mwaka 2005 Mkoa ulikuwa na Wilaya 3, Halmashauri 4 (moja ya Manispaa na 3 za Wilaya), Tarafa 19, Kata 85, Vijiji 229, Mitaa 199 na Vitongoji 1,343. Kwa sasa Mkoa una Wilaya 6, Halmashauri 8 (moja ya Manispaa, moja ya Mji na sita za Wilaya), Tarafa 21, Kata 136, Vijiji 306, Mitaa 176 na Vitongoji 1,856. Ongezeko hilo lina maana kwamba usimamizi unazidi kuimarika na huduma zimesogezwa karibu zaidi na Wananchi.
IDADI YA WATU
Kwa mujibu wa sensa ya Watu na makazi iliyofanyika mwaka 2012, Mkoa wa Kigoma ulikuwa na watu wapatao 2,127,930. Kati ya hao Wanawake ni 1,098,936 na Wanaume ni 1,028,994. Idadi hii ya watu inaongezeka kwa wastani wa asilimia 2.4 ikilinganishwa na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002. Kwa sasa Mkoa wa Kigoma unakadiriwa kuwa na idadi ya Watu 2,297,927.
ENEO LA MKOA.
Mkoa wa Kigoma una eneo la kilomita za mraba 45,075. Kati ya hizo, kilomita za mraba 36,523 ni nchi kavu na kilomita za mraba 8,552 ni eneo lililofunikwa na maji. Mkoa unapakana na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) upande wa Magharibi na Burundi upande wa Kaskazini Magharibi. Ndani ya nchi, Mkoa unapakana na Mikoa ya Kagera upande wa Kaskazini, Shinyanga upande wa Kaskazini-Mashariki, Katavi na Rukwa upande wa Kusini na Tabora upande wa Mashariki. Kwa kiasi kikubwa kuanzia Kaskazini Mashariki yote mpaka Kusini Mashariki Mkoa umezungukwa na Ziwa Tanganyika.
HALI YA HEWA.
Hali ya hewa ya Mkoa wa Kigoma ni ya joto kiasi na unyevunyevu. Joto linafikia nyuzi joto kati ya 17–33‘centigrade’ na unapata wastani wa mvua zenye ujazo wa mm 800 – 1200 kwa mwaka. Kutokana na mvua za kuaminika, wakulima huweza kupanda baadhi ya mazao hadi mara mbili kwa mwaka. Mvua huanza mwezi Oktoba na kuishia mwezi Mei na kufuatiwa na kipindi kirefu cha jua yaani kiangazi.
SHUGHULI KUU ZA KIUCHUMI.
Shughuli kuu za kiuchumi katika Mkoa wa Kigoma zimejikita katika maeneo makuu yafuatayo: Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Biashara na Viwanda vidogovidogo. Kilimo kwa kiasi kikubwa bado kinaendeshwa kwa kutumia jembe la mkono. Aidha, baada ya kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo kumekuwa na ongezeko la matumizi ya matrekta makubwa na madogo. Jitihada za Uongozi wa Mkoa na ongezeko la kibajeti, rasilimaliwatu na vitendea kazi uliofanywa na Serikali umewezesha changamoto nyingi kutatuliwa na hivyo kuwapa fursa Wananchi kujikita katika uzalishaji mali.
PATO LA MKOA NA PATO LA MWANANCHI.
Kutokana na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kijamii na kiuchumi katika Mkoa, pato la Mkoa (Gross Domestic Product) linaendelea kupanda kutoka shilingi milioni 575,350 mwaka 2006 hadi shilingi milioni 2,261,038 mwaka 2014. Aidha, pato la Mwananchi (Per Capital Income) wa Mkoa wa Kigoma pia linaendelea kuimarika kutoka Tshs. 291,946 mwaka 2006 hadi kufikia Tshs. 1,012,774 mwaka 2013. Viwango hivi ni kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu