Ujenzi wa Mitaro ya Maji katika Manispaa ya Kigoma Ujiji umetajwa kunusuru Nyumba 384 zilizokuwa hatarini kuathiriwa na maji kutokana na kupakana na Makorongo au maeneo yanayopitisha maji kwa wingi nyakati za Mvua.
Hayo yamebainishwa wakati za ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro alipotembelea Miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Kiushindani Tanzania (TACTIC) inayotekelezwa Katika Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani hapa.
Akizungumza mara baada ya kukagua miradi hiyo, Balozi Sirro amesema miongoni mwa kazi zinazotekelezwa kupitia mradi ni udhibiti wa athari za makorongo saba ambapo unafanyika ujenzi kuimrisha kingo zake ili zisizidi kutanuka na kuleta madhara kwenye makazi.
Aidha, Sirro amewataka wakazi katika manispaa hiyo kutoigeuza mitaro hiyo kuwa maeneo ya kutupa takataka, jambo linaloweza sababisha ishindwe kupitisha maji kwa usahihi.
Katika hatua nyingine Balozi Sirro amesisitiza ukaguzi wa mara kwa mara wa miradi hiyo ili iweze kutekelezwa na kukamilika kuendana na matakwa ya kimkataba.
Upande wake Mhandisi wa TARURA Mkoa Ellius Mutapima amesema ujenzi wa mitaro unakwenda sambamba na ujenzi wa daraja katika mto Ruiche pamoja na barabara ya Ujiji-Bangwe kwa Thamani ya Shilingi Bil. 29.8.
Pia Mha. Mutapima amewataka wananchi wanaokaa katika maeneo inamopita mitaro hiyo, kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza jitokeza hususani watoto kutumbukia katika mitaro hiyo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa amekagua pia ujenzi wa Soko la Mwanga, Katonga pamoja na mtaro wa kuondoa maji katika eneo la Katubuka huku akionesha kuridhishwa na kazi zinavyoendelea kufanyika.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa