Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amekabidhi magari manne yaliyotolewa na Serikali kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma huku akitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa wakati kuhusu uwepo wa matukio ya ajali za moto na matukio mengine yanayoshughulikiwa na jeshi hilo.
Amesema, mara baada ya kupokea vitendea kazi hivyo, Jeshi hilo linapaswa kuongeza ufanisi kiutendaji kazi huku akisisitiza utunzaji wa magari na vifaa vingine vilivyopokelewa ili viweze kufanya kazi kwa muda mrefu.
"Pamoja na ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha, Jeshi hili limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kupata mafanikio makubwa kila ilipohitajika kufanya hivyo. Nichukue fursa hii kuwapongezeni kwa kazi nzuri mnazofanya" amesema Sirro.
Aidha Balozi Sirro ameishukuru serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi hivyo, jambo litakaloimarisha utendaji kazi wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa ametoa rai kwa Jeshi hilo kutumia vyombo hivyo kwa lengo la kuleta mapinduzi katika eneo lao la utendaji kazi wao.
Amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wa jeshi hilo watahakikisha nyenzo hizo zinatumika kwa kuzingatia malengo ya serikali.
Awali akitoa taarifa ya mapokezi ya vifaa hivyo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kigoma Michael Maganga, amesema vitendea kazi walivyopokea ni pamoja na mtambo wa kisasa wa kuzima moto, gari la kubeba maji, gari la operesheni na gari la wagonjwa.
Ametoa wito kwa wananchi mkoani hapa kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa mapema ili liweze kufika maeneo ya matukio kwa wakati jambo litakalofanikisha kupunguza athari za majanga.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa