Wakazi wa kata ya Makere wilayani Kasulu mkoani Kigoma wameishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa Kituo cha Afya wilayani humo hali itakayowaondolea adha ya muda mrefu ya ukosefu huduma za afya kwa ukaribu na kusababisha kwenda kutibiwa maeneo ya mbali huku baadhi yao wakipatiwa matibabu katika Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani humo.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa Thamani ya Shilingi Bil 1.66 kupitia miradi ya nyongeza itokanayo na ujenzi kwa barabara kwa kiwango cha lami Kabingo, Kasulu hadi Manyovu chini ya Ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025 ukihusisha ujenzi wa jengo la Utawala, wazazi, upasuaji, Maabara, jengo la kuhifadhia maiti, ufuaji pamoja na jengo la makazi ya mtumishi.
Method Erick ambaye ni mkazi wa kata hiyo amesema mara nyingi zinapotokea changamoto za kiafya kwa wakazi katika eneo hilo na jirani wamekuwa wakitegemea kituo cha Afya kilichopo katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu ambapo wamekuwa wakichelewa kupata huduma kutokana mchakato wa kupata vibali ili kuingia kambini humo jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha ya wagonjwa mahututi pamoja na wanawake walio katika hatua ya kujifungua.
Peter Basilia Mkazi wakijiji cha Nyangwa kata ya Makere, amesema awali kwa sasa tegemeo kuu la matibabu katika kata hiyo ni Zahanati ya kijiji pekee huku eneo hilo likiwa na idadi kubwa ya wakazi, hali inayosababisha kituo hicho cha kutolea huduma ya afya kuwa na foleni kubwa ya wagonjwa huku kikiwa na idadi ndogo ya watendaji na vifaa visivyokidhi mahitaji ya kitabibu.
Amesisitiza kuwa, kituo hicho kitapunguza au kuwaepusha kabisa na gharama za kusafirisha wagonjwa ili kuwafikisha katika vituo vingine vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali za Wilaya na mji Kasulu au Hospitali ya Rufaa ya Kabanga iliyopo wilayani humo.
Naye Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Dkt. Joseph Tubeti amesema mradi utakapokamilika utaongeza fursa za upatikanaji huduma za afya za msingi, upasuaji kwa mama watakaopata changamoto ya uzazi pingamizi pamoja na huduma ya kuhifadhi miili inapotokea vifo.
Amesema kata ya makere inakadiriwa kuwa na wakazi Zaidi ya Sitini elfu hivyo uwepo wa huduma hiyo utapunguza mzigo kwa vituo jirani vya kutolea huduma za afya. Aidha amesisitiza kuwa kwa sasa hali ya upatikanaji vifaa tiba imezidi kuimarika hali inayochangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa ufanisi katika kukabiliana na maradhi wilayani humo.
Aidha Dkt. Tubeti ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya uwepo wa ongezeko la vituo vya kutolea huduma za Afya kuejenga tabia ya kujitokeza na kupima afya zao mara kwa mara ili kuepukana na matibabu ya muda mrefu yatokanayo na usugu wa maradhi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa