Zoezi la umezeshaji dawa za kinga-tiba dhidi ya Magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo.
Posted on: May 19th, 2017
Viongozi wa kidini na waandishi wa Habari Mkoani Kigoma wameombwa kushirikiana na Serikali kuwaelimisha wananchi katika zoezi la umezeshaji dawa za kinga-tiba dhidi ya Magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo.
Haya yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Daniel Machuda katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa wa Kigoma kilichoketi kujadili juu ya utekelezaji wa zoezi la umezeshaji wa dawa za kinga-tiba dhidi ya magonjwa yaliokuwa hayapewi kipaumbele. Zoezi la umezeshaji umezeshaji dawa za kinga-tiba dhidi ya Magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya tumbo litazinduliwa katika shule ya Msingi Simbo Mkoani Kigoma siku ya tarehe 24 Mei, 2017.
Machunda alisema hakuna Serikali inayoweza kuwapatia wananchi wake dawa za kuwadhuru hivyo wazazi na jamii yote wasiwe na hofu juu ya dawa hizo zenye lengo la kuokoa afya za watoto kwa vizazi vijavyo.
Akitoa taarifa ya zoezi la umezeshaji wa dawa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Paulo Chaote alisema mwaka 2016 zoezi hilo lilighubikwa na uvumi wa uongo kwa baadhi ya maeneo Mkoani Kigoma na kusababisha watoto wengi kutopata dawa kama ilivyokuwa imepangwa na Wizara ya Afya,maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto.
Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yameelezwa kuwa yanasababisha madhara Makubwa kwa jamii kwani huambukizwa kirahisi. Katika zoezi la umezesaji Mkoa wa Kigoma umelenga kuwapatia dawa watoto walioko shule za Msingi kwani kutokana na tafiti zilizofanyika magonjwa hayo huwaingia watoto kirahisi zaidi.