Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Kigoma wametakiwa kufuata Sheria ili kuepuka Makosa yanayotoa fursa kwa baadhi ya Askari wa Usalama Barabarani wasiokuwa waadilifu kuyamaliza makosa hayo nje ya taratibu za kisheria kwa kupokea Rushwa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alipozungumza na wamiliki wa mabasi na madereva kwenye Mkutano Mkuu wa wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Kigoma (KIBOTA) uliofanyika leo Mei 6, 2023 katika Ukumbi wa Joy in the harvest Mjini Kigoma.
Amesema iwapo vyombo vya usafiri vitaimarishwa ili kutokuwa na dosari pamoja na madereva kuongeza umakini na kuzingatia Sheria zinazoongoza utendaji kazi wao, itasaidia kupunguza makosa ya Barabarani yanayotoa nafasi ya uwepo wa mianya ya rushwa kwa baadhi ya Askari wasio waadilifu wenye jukumu la kusimamia usalama barabarani.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewaelekeza wadau hao muhimu wa usafirishaji wa Abiria, kuisaidia Serikali katika kudhibiti wimbi la wahamiaji Haramu katika Mkoa kwa kutoa taarifa katika Mamlaka husika wanapobaini uwepo wa raia wa kigeni kwenye vyombo vyao vya usafiri ili taratibu na hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa lengo la kuimarisha usalama wa Nchi.
Amesema baadhi ya wamiliki pamoja na madereva wa magari madogo ya kusafirisha abiria wamekuwa wakikodiwa kwa ajili ya kusafirisha Raia wa Kigeni kinyume na Sheria, Jambo linaloipa wakati mgumu Serikali kupitia Jeshi la Uhamiaji kubaini na kudhibiti uingiaji holela wa raia wa kigeni nchini.
Mkutano huo umehudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Afisa Biashara, TAKUKURU (M) Kigoma pamoja na Meneja wa TANROADS, TARURA na LATRA ambapo wajumbe wamepata fursa ya kuuliza maswali kwa wageni waalikwa na kupata ufafanuzi wa Hoja zao kisha wameendelea na kikao chao cha kisheria.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa