NA. CLINTON JUSTINE-KIGOMA RS
Kukamilika kwa Ujenzi wa Kituo cha Afya Rukoma wilayani Uvinza Mkoani Kigoma kutawaondolea adha wakazi wa kijiji hicho kutembea umbali wa zaidi ya Kilomita Kumi kufuata huduma za Afya katika Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Buhingu wilayani humo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa Kijiji hicho wamesema kituo kitakapokamilika kitasaidia kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, watoto na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali kutokana na kutumia muda mfupi kufika katika kituo hicho tofauti na sasa ambapo hulazimika kusafirisha wagonjwa wao umbali mrefu kwa kutumia usafiri wa pikipiki ili kuzifikia huduma za Afya.
“Ukamilishwaji wa kituo cha hiki utasaidia kupunguza gharama za kusafirisha wagonjw sambamba na kupunguza vifo kwa wajawazito, wazazi, watoto na kwa wagonjwa wenye maradhi mbalimbali ’’ amesema Shabani Saidi Afisa Mtendaji kijiji cha Rukoma.
Hamis Kasanga ambaye ni mkazi kijijini hapo amesema upatikanaji wa uhakika wa huduma za afya katika eneo hilo, utabadilisha mtazamo wa wakazi na kuwaondolea fikra na Imani za kishirikina katika kutatua changamoto zao za kiafya kutokana na upatikanaji wa vipimo vya Afya na kuweza kubaini maradhi katika hatua za awali.
‘‘kutokana na umbali katika kuzifikia huduma za Afya na kuepuka kutumia gharama kubwa, baadhi ya wakazi wamekuwa wakitumia tiba asili na kujihusisha na waganga wa kienyeji sambamba na kutumia ramli chonganishi pale wanaposumbuliwa na maradhi’’ amesema Hamis Kasanga.
Upande wake Joseph Kihanda ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amesema kumekuwa na changamoto za kiusalama zinazowakumba madereva wa pikipiki wanaposafirisha wagonjwa nyakati za usiku ikiwemo kuporwa vyombo vyao vya usafiri sambamba na kujeruhiwa.
Naye Tumaini Paulo ambaye ni mkazi kijijini hapo ,amesema kukamilika kwa kituo cha afya rukoma kitasaidia kuokoa maisha ya wakazi wa eneo hilo kwa kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga
Aidha ameiomba serikali kuongeza kasi katika ukamilishwaji wa kituo hicho ili upatikanaji wa huduma uweze kuanza mara moja.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa