Mkuu wa Mkoa wa Kigoma CGF (Mst) Thobias Andengenye, amegawa zawadi zilizotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa makundi mbalimbali mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani hapa.
Kabla ya kugawa zawadi hizo, Mkuu huyo wa Mkoa alipata fursa ya kuzungumza na waumini wa madhehebu ya kiislam katika msikiti wa Muumin uliopo Manispaa ya Kigoma-Ujiji, ambapo amesema zawadi hizo zimeonyesha ni kwa jinsi gani Mhe. Rais anaguswa na kutambua uwepo wa makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na maendeleo ya mkoa wa Kigoma.
Amesema Rais anaendelea kuweka mazingira yenye tija kwa maendeleo ya wanakigoma ambapo meidhinisha kufanyika kwa ujenzi wa Hospitali ya Kanda pamoja na Tawi la Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Muhimbili, ambavyo vitafungua fursa mbalimbali za kibiashara kutokana na kuongezeka kwa muingiliano wa watu.
‘‘Nashauri wanakigoma mjiandae kuchangamkia fursa kuendana na mahitaji yatakayojitokeza mara baada ya kukamilika kwa miradi hiyo ili muweze kujiinua kiuchumi’’ Amesema.
Akiwa katika Kituo cha kuwahudumia watoto waliokosa wazazi na wenye changamoto za kimalezi Sanganigwa B, Mkuu wa Mkoa amesema mbali ya kutoa misaada hiyo kwa niaba ya Mhe. Rais, Serikali mkoani hapa itaendelea kutoa misaada mbalimbali ili kuhakikisha watoto hao wanatimiza ndoto zao.
‘‘Nasisitiza mnaobeba jukumu la kuwalea watoto hawa, muwe mnawasimulia Historia mbalimbali za watu waliowahi kupitia mazingira kama wanayoyaishi kisha wakafanikiwa na kutimiza ndoto zao ili waweze kuamini katika kutimiza ndoto zao na kuongeza bidii bila kukatishwa tamaa’’
Pamoja na zawadi ya vifaa vya Ibada vilivyotolewa kwa Shehe Mkuu wa Mkoa katika Msikiti wa Muumin-Ujiji, zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na vifaa vya kitaaluma, vyombo vya chakula, mafuta ya kula na mchele ambavyo pia vitaendelea kutolewa katika vituo vya Bangwe, MWOCACH, Makao ya wazee (Kibirizi), kituo cha JUVENILE pamoja Kituo cha watoto Matiazo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa