Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI inatarajia kuanza kutoa chanjo ya Polio kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo katika Nchi jirani za Malawi na Zambia.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema mpaka sasa wamepokea Jumla ya chanjo 761,240 kwa lengo la kuchanja watoto wote walio na umri chini ya Miaka mitano ikiwa ni pamoja na waliopo katika kambi za wakimbizi kutoka Nchi za Kongo na Burundi.
Zoezi la utoaji chanjo linatarajiwa kuanza Tarehe 1 hadi 4 Mwezi Sepemba 2022 ambapo litafanyika nyumba kwa nyumba, katika vituo vya kutolea huduma za Afya, huduma ya Mkoba na maeneo mengine ya Mikusanyiko na litawahusu waliochanjwa na wale ambao hawajawahi kuchanjwa.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wanahabari, wasanii, viongozi wa dini, wadau wa Afya na Wananchi kuendelea kutoa Elimu na kuhamasishana kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo kwa watoto ili kuwakinga na janga la Polio ambalo limeshaathiri baadhi ya Nchi za jirani.
Naye katibu Tawala Mkoa, Msovela Gabriel amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia matumizi ya chanjo hiyo ili kupunguza au kuepuka kabisa athari zitakazoweza kujitokeza siku za usoni na kusababisha madhara makubwa kwa Taifa.
Amesema mbali ya kuelimishwa, Jamii haina budi kutambua jukumu la ulinzi wa Afya ni la kila mtu, hivyo Wananchi waone umuhimu wa kuiunga mkono Serikali katika kuchukua tahadhari kuliko kusubiri kukabiliana na athari za maradhi hayo.
Mkoa wa Kigoma unamuingiliano mkubwa wa Raia kutoka Nchi jirani kupitia Ziwa Tanganyika, jambo linaloweza kurahisisha kuenea kwa maradhi hayo nchini kutokana na Nchi ya Zambia kukumbwa na mlipuko wa Polio.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa