Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa SAMIA SULUHU HASSAN amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kanda Mkoani Kigoma ambayo itahudumia wakazi mkoani hapa pamoja na Mikoa jirani ya Katavi na Tabora.
Mhe. Rais ametoa Kauli hiyo wakati akiweka jiwe la Msingi kwenye jengo la msaada wa dharura pamoja na jengo la wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Rufaa ya Maweni -Kigoma, ambapo majengo hayo yamegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 kutoka serikali Kuu.
Amesema lengo la ujenzi wa hospitali hiyo ni kutoa matibabu ya kisasa pamoja na utalii wa kiafya kwa wananchi wa ndani na nje ya nchi ya Tanzania zikiwemo nchi jirani kutokana na Mkoa wa Kigoma kuwa kimkakati kijamii, kibiashara na kiutamaduni.
Aidha Mhe. Rais ameahidi kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni Mbili kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo mbalimbali katika Hospitali hiyo ili kuwezesha utendaji kazi wenye ufanisi.
Awali, Mhe. Rais Samia ameweka Jiwe la Msingi katika eneo la Ujenzi wa Bandari ndogo ya Kibirizi unaotekelezwa kwa Fedha kutoka Serikali Kuu wenye Thamani ya Shilingi Bil. 32, ukihusisha ujenzi wa gati, ofisi za wafanyakazi, eneo la kupumzikia abiria na Ghala la kuhifadhia Mizigo.
Pia, Rais Samia amewataka wakazi hao wa Kata ya Kibirizi kuupokea mpango wa Serikali wa ujenzi wa Soko la kisasa katika eneo hilo kwa kuruhusu ubomoaji vibanda vilivyojengwa bila kufuata mpangilio ili kulifanya eneo hilo kuwa katika mpangilio mzuri tofauti na lilivyo kwa sasa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa