WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI NAPE NNAUYE AKISALIMIANA NA MKUU WA MKOA WA KIGOMA THOBIAS ANDENGENYE MARA BAADA YA KUWASILI KATIKA OFISI YA MKUU WA MKOA WA KIGOMA KWA AJILI YA ZIARA YA KIKAZI YA KUKAGUA MAENDELEO YA SEKTA YA MAWASILANO MKOANI HAPA.( KULIA NI KATIBU TAWAL MKOA WA KIGOMA HASSAN RUGWA)
Waziri wa Habari, Mawasiliano ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye ametembelea na kuzindua minara ya Mawasiliano katika vijiji vya Kumbanga na Bunyambo vilivyopo wilayani Kibondo mkoani hapa na kuwataka wananchi kutumia fursa ya maboresho makubwa ya miundombinu hiyo kwa lengo la kujiletea matokeo chanya kwenye Nyanja ya mawasiliano.
Minara hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa minara 758 inayojengwa na Serikali nchini kupitia Ruzuku kutoka mfuko wa Mawasiliano kwa wote (USCAF) ambapo kwa mkoa wa Kigoma utekelezaji wa ujenzi huo unafanyika katika Halmashauri ya Kasulu, Kibondo na Uvinza na hadi kufikia Juni 2024, jumla ya Shilingi Bil. 1.38 zimetumika kujenga minara hiyo katika kata 8 zenye vijiji 10 huku wakazi 108,126 wakitarajiwa kuanza kunufaika.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa kijiji cha Kumbanga na Bunyambo, Waziri Nape amesema kati ya minara hiyo nane (8) yenye uwezo wa kutoa huduma za kimtandao za 2,3 na 4G inayojengwa mkoani hapa, tayari minara mitatu(3) imekamilika na imeanza kufanya kazi katika wilaya ya Uvinza na Kibondo kwenye vijiji vya Katete, Kumbanga na Bunyambo.
Waziri Nape amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua hali ya maendeleo ya mawasiliano mkoani Kigoma ambapo serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa uhakika katika maeneo yote kwa ubora ili kuleta matokeo chanya kwa watumiaji ambao ni wananchi wote wa Tanzania.
Nape amewataka wakurugenzi watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani hapa kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha upatikanaji wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa minara sambamba na vibali vya kumiliki maeneo hayo vinapatikana kwa wakati.
‘‘Nizielekeze Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mtumie wataalam wenu kufanya utafiti na kubaini maeneo yote yenye uhitaji wa mawasiliano na kuwasilisha taarifa hiyo kwa wizara kupitia Mamlaka ya Mawasiliano nchini ili serikali iweze kuweka mipango kwa ajili ya kufikisha huduma hiyo muhimu kwa wananchi’’ amesisitiza Waziri Nape.
Aidha Waziri huyo amewataka wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha anafikisha miundombinu ya Umeme na Barabara kwa ajili ya uendeshaji wa minara hiyo ili iweze kufanya kazi kwa wakati bila mikwamo yoyote ya kiutendaji na kuruhusu huduma kuwafikia wananchi kama ilivyopangwa.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuzingatia matumizi bora ya mawasiliaano ikiwemo kujisali kwa usahihi, kuepeuka kutoa taarifa za uongo ikiwemo kufanya utapeli wa mtandaoni sambamba na kutumia mitandao hiyo kwa malengo chanya badala ya kutoa taarifa zenye upotoshi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa Amani ndani ya jamii na nchi kwa ujumla.
Akitoa Salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema Serikali mkoani hapa ipo tayari kuendelea kutoa ushirikiano na Wizara hiyo ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi na zikiwa endelevu.
Idha katika kuhakikisha wananchi wanatekeleza takwa la kisheria la kujisajili kikamilifu katika mifumo ya mawasiliano, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kufuatilia vitambulisho vyao vya Taifa katika maene elekezwa kutokana na wengi wao kushindwa kuvifuata kwa wakati huku serikali ikiwa imekamilisha zoezi la utoaji wa vitambulisho hivyo.
Aida ametoa wito kwa wakazi mkoani hapa kuendelea kunufaika na huduma za mawasiliano ikiwemo kujiajiri kupitia huduma za kifedha, kutumia mitandao kwa ajili ya kujijengea uwezo na kujiimarisha kitaaluma sambamba na kutumia haki yao ya kupokea na kutuma taarifa mbalimbali.
Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Kumbanga na Bunyambo wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanikisha ufikishaji wa huduma hiyo muhimu ya mawasiliano katika vijiji vyao.
Wamesema awali katika vijiji hivyo wananchi walikuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo uwepo wa mashambulizi ya wanyama wakali na maradhi huku wakishindwa kuwasiliana kwa wakati ili kupata msaada na kujinusuru na changamoto hizo.
‘’Ilikuwa inatulazimu kutembea hadi vijiji vya jirani ikiwa ni zaidi ya Km 20 ili kufikia maeneo ambayo tunaweza kufanya mawasiliano na ndugu au njamaa zetu lakini kwa sasa mawasiliano yametufikia na hatutokutana na changamoto hizo tena’’ amesisitiza Zena Kalihose mkazi wa kijiji cha Kumbanga.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa