Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb)amesema ameridhishwa na matumizi ya Fedha zaidi ya Shilingi Tril.11 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo mkoani Kigoma.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo alipozungumza mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya Siku tatu mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa pamoja na matumizi mazuri ya fedha hizo yapo maeneo hakuridhika na utekelezaji wa miradi kutokana na kukwamishwa na wasimamizi wa miradi hiyo jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha maendeleo ya wananchi.
Amesema katika maeneo yote aliyobaini baadhi ya watendaji wa Serikali kutumia kinyume na utaratibu fedha zinazotolewa na Serikali, ametoa maelekezo sambamba na kuchukua hatua dhidi ya watendaji walioshiriki kukwamisha miradi ya serikali.
‘’Tunakwenda kukutana na watendaji wenzangu walio chini ya wizara hii ili kuandaa Taarifa kamili kwa ajili ya kuchukua hatua katika maeneo yote ambayo watendaji hawakufanya vizuri kwa sababu za kushindwa kuwajibika’’ amesema Waziri.
‘’Nasisitiza hata kama mtumishi amehitimisha muda wake wa utumishi serikalini, amehamishwa au uteuzi wake umetenguliwa tutamrejesha hapa ili aweze kujibu makosa yake iwapo tutathibitisha kuwa mtumishi huyo alishiriki kupokea rushwa, kusababisha ubadhirifu au aina yoyote ya upotevu wa fedha za serikali hatutosita kuchukua hatua’’amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Mchengerwa ametoa wito kwa viongozi wote wa serikali kukumbuka wao ni watumishi wa wananchi, hivyo watumie nafasi zao kuwatumika watanzania. Ukiwa waziri, Mkuu wa Mkoa, mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi nk, jitahidi kuwatumikia wananchi ili uweze kuacha alama kwa unaowatumikia na Taifa kwa ujumla.
Awali waziri huyo amekagua jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Uvinza na kuielekeza TAKUKURU kufanya uchunguzi kuhusiana na ujenzi wa jengo la ofisi hiyo kutokana na waziri huyo kubaini baadhi ya kazi zilizofanyika katika ujenzi wa jengo hilo kutozingatia miongozo ya serikali na kukosa ubora.
Aidha amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha ndani ya Siku mbili kuanzia Agosti 14, 2024, jengo hilo linaunganishwa kwenye mfumo wa Umeme ili kurahisisha utendaji kazi wa watumishi wanaotumia ofisi hiyo.
Akiwa katika shule ya sekondari ya Uvinza Wasichana, Mhe. Mchengerwa amemuelekeza mhandisi wa Wilaya hiyo kuhakikisha huduma ya Umeme inafika kwenye mabweni yote ya shule hiyo.
Aidha Mchengerwa amepata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo na kusisitiza kuwa Mhe. Rais anaguswa na changamoto ya upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa kike ndio maana akaanzisha utaratibu wa kujenga shule hizo ili kuweza kuwapa fursa wasichana kupata elimu bora.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa