Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) amememuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini nchini TARURA Mkoa wa Kigoma kuweka taa katika barabara zote zinazojengwa na wakala huyo mkoani Kigoma ili kudumisha usalama nyakati za usiku sambamba na kupendezesha miji katika maeneo zilipo barabara hizo.
Mhe. Waziri Mchengerwa ametoa maelekezo hayo alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami Km. 1.1 kutoka Ujenzi hadi GTZ na Kiganamo hadi Bogwe katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Amesema Mhe.Rais Dkt. Samia amelenga kuendelea kuimarisha miundombinu ya barabara mkoani Kigoma ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kupitia sekta hiyo muhimu ya uchukuzi sambamba na kuboresha mazingira ya miji katika mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
Ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami nyepesi umegharimu kiasi cha Shilingi Mil. 950, fedha kutoka serikali kuu na kukamilika kwake kumetajwa kuwaondolea adha ya ubovu wa barabara wakazi wa mji huo na kuzifanya zipitike kwa wepesi nyakati za masika na kiangazi.
Awali akiwa waziri huyo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mwami Ntale kilichopo katika Halmashauri hiyo na kumuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo kumbadilishia Kituo cha Kazi Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kasulu Dkt.Peter Janga kutokana na kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.
‘’Haiwezekani kituo kifunguliwe na kukosa Samani kwa kipindi cha zaidi ya Mwaka, huku kikiwa hakina Umeme na majengo kutotosheleza, hii haikubaliki na nnakuagiza Katibu Mkuu kumbadilishi kituo cha kazi sambamba na kuitaka TAKUKURU kufika hapa na kuanza uchunguzi wa ujenzi wa mradi huu’’amesema mchengerwa.
Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa ameiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi katika Shule ya Sekondari Nyumbigwa Mpya kupitia Program ya P4R kwa kiasi cha Shilingi Bil. 1 na fedha hizo kumalizika huku baadhi ya miundombinu ya Shule ujenzi wake kutokuwa umekamilika.
Kupitia ziara hiyo, Waziri Mchengerwa amesikiliza na kupokea kero za wananchi katika kata ya Kagerankanda ikiwemo uwepo wa changamoto ya uwepo wa migogoro ya ardhi, kata hiyo kutokuwa na diwani tangu mwaka 2021 sambamba na ombi la kupandishwa hadhi kwa shule ya sekondari kimenyi hadi kufikia kidato cha Sita.
Akitoalea ufafanuzi jero hizo za wananchi, Waziri huyo ameahidi kupeleka wataalam kutoka Wizara hiyo wanaoshughulikia masuala ya Elimu ili kuona kama Shule hiyo ya Sekondari ya Kimenyi inakidhi vigezo vya kupandishwa hadhi hadi kutoa Elimu ya Kidato cha Sita.
Sambamba na hilo, waziri Mchengerwa ameahidi kukutana na Diwani wa Kata hiyo aliyesimamishwa kwa changamoto za masuala ya uraia ili kufahamu kiwango cha utatuzi wa changamoto zake ili aweze kurudi kuwatumikia wananchi.
Kuhusu suala la migogoro ya ardhi, Mchengerwa ameahidi kurudi katia kata hiyo ndani ya kipindi cha Siku 30 akiwa na Waziri mwenye dhamana ya ardhi ili kutatua na kuzitolea maamuzi changamoto ambazo wananchi hao wanankutana nazo kupitia sekta hiyo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa