WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI. MHANDISI HAMAD MASAUNI AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI MARA BAADA YA KUFUNGA KIKAO CHA PANDE MBILI KILICHOWAHUSISHA WATAALAM KUTOKA NCHI ZA TANZANIA NA BURUNDI KWA AJILI YA KUJADILI NA KUWEKA MIKAKATI YA PAMOJA YA UTEKELEZAJI WA ZOEZI LA UREJEAJI WA WAKIMBIZI KUTOKA NCHINI BURUNDI.
WAZIRI MASAUNI(KATIKATI) AKIFUATILIA JAMBO WAKATI KIKAO HICHO KIKIENDELEA. WA KWANZA KUSHOTO NI MKUU WA MKOA WA KIGOMA THOBIAS ANDENGENYE, NA WATATU KULIA NI MWAKILISHI KUTOKA SERIKALI YA BURUNDI THEOPHILE NDARUFATIYE.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kutumia utaratibu wa hamasa katika kuhakikisha wakimbizi kutoka Burundi wanarejea nchini humo kutokana na kuimarika kwa hali ya Amani na utulivu.
Waziri Masauni ametoa Kauli hiyo alipozungumza wakati akifunga Kikao cha wataalam walioziwakilisha nchi za Tanzania na Burundi, kilichofanyika mkoani hapa kwa lengo la kujadili urejeaji wa wakimbizi hao na kusisitiza kuwa jitihada hizo zisitafsiriwe kuwa ni chuki bali ni dhamira ya serikali zote mbili kuwataka wakimbizi hao kurejea nchini humo kwa jili ya kujenga nchi yao.
Amesema lengo la serikali hizo mbili ni kuhakikisha linapatikana suluhisho la kudumu ili wakimbizi waweze kurejea nchini Burundi kwa hadhi, usalama na upendo kupitia utaratibu wa Hamasa utakaowawezesha kupata fursa za kifedha sambamba na vifaa vitakavyowasaidia kuanza maisha nchini humo.
‘‘Kwa sasa tupo katika kipindi cha hamasa kwa ajili ya urejeaji wa hiyari mpaka itakapofika Mwishoni mwa mwezi Desemba 2024, baada ya hapo mpango huo usipokamilika, wakimbizi hao watakuwa wamepoteza hadhi ya ukimbizi hivyo litafuata zoezi la kuwahoji na kufahamu sababu za kila mmoja kuendelea kuwepo nchini ili kuona kama zitaendelea kumpa sifa ya kuwa mkimbizi’’ amefafanua Mhandisi Masauni.
Waziri huyo amesisitiza kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kushughulikia masuala yote yanayowahusu wakimbizi kwa kuheshimu na kuzingatia Sheria na Mikataba yote iliyopo kikanuni ili kuweza kuwarudisha wakimbizi hao nchini mwao kwa heshima na staha.
Aidha Waziri Masauni amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kufanya jitihada kubwa zilizosababisha mkoa wa Kigoma kuendelea kuwa katika hali ya usalama, Amani na utulivu.
Upande wake Mwakilishi wa Serikali ya Burundi Theophile Ndarufatiye amesema idadi ya wakimbizi wanaorejea nchini humo ni ndogo sana jambo lililowasukuma kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuendelea kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha kasi ya urejeaji kwa hiyari inaongezeka.
‘’Tangu mwaka 2017 hadi kufikia 2024 jumla ya wakimbizi 1,070,607 wamerejea nchini Burundi ambapo kwa mwaka 2024 hadi kufikia Mei 31, jumla ya wakimbizi 5,709 wamerejea huku zaidi ya wakimbizi laki moja bado wanaendelea kupatiwa hifadhi katika kambi za Nyarugusu na Nduta’’ amesema Ndarufatiye.
Mwakilishi huyo ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuwakarimu raia hao wa nchi hiyo huku akisisitiza kuwa wakimbizi watakaorejea kwa hiyari nchini humo kupitia mpango wa hamasa watapatiwa kiasi cha fedha kwa ajili ya kujikimu, huduma za vyeti vya uraia na ndoa, watoto wao kupelekwa shule, kupatiwa makazi, vifaa vya ujenzi pamoja na huduma nyinginezo muhimu za kijamii.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa