Waziri Dkt. Selemani Jafo akiwa na viongozi wa Serikali Mkoa wa Kigoma mara baada ya kukagua eneo la Mlima Mlole katika Mtaa wa Sanganigwa Manispaa ya Kigoma-Ujiji ambalo hapo awali Serikali ilisitisha uendelezaji wa Makazi pamoja na shughuli nyinginezo za kibinaadamu kutokana na uwepo wa atahari kubwa za kimazingira.Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Gabriel Msovela (wakwanza kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Kigoma CGF(Mst) Thobias Andengenye pamoja na Waziri Dkt. Selemani Jafo wakifurahia jambo na wananchi (hawapo pichani) mara baada ya kumaliza kuzungumza na Wakazi wa Mtaa wa Sanganigwa na kuwaruhusu kuendelea na shughuli za uendelezaji wa makazi katika eneo la Mlima Mlole.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Dkt. Selemani Jafo, ameidhinisha uendelezaji wa Makazi katika Eneo la Mlima Mlole Kata ya Sanganigwa, Manispaa ya Kigoma-Ujiji mkoani Kigoma ambapo awali Serikali ilisitisha shughuli hizo ili kuchunguza iwapo zingeweza kuleta Athari za kimazingira katika Bandari ya Kigoma.
Waziri Jafo amesema Serikali kwa kutumia Wataalam wa Bandari pamoja na Mazingira wamejiridhisha kutowepo kwa Athari hizo kwa sasa kutokana na uimarishwaji wa kuta za mto Rubengela uliokuwa ukisababisha mmomonyoko wa Ardhi nyakati za mvua katika eneo hilo na kupelekea tope na mchanga mwingi kuingia eneo la bandari na kuathiri ufanisi katika utendaji kazi.
Amri ya zuio la kuendeleza makazi ilitolewa na mamlaka ya usimamizi wa Bandari mkoani Kigoma Mwaka 2009 ambapo wakazi wa eneo hilo walitakiwa kusitisha ujenzi wa nyumba pamoja na shughuli nyingine za kibinaadamu ili kusubiri kufanyika kwa utafiti ambao ulisababisha Serikali kuja na jibu la ujenzi wa kingo za Mto huo hali iliyopunguza mmomonyoko wa Ardhi katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Uzimamoto na Uokoaji, Mhe.Thobiasi Andengenye amemshukuri Waziri Jafo kwa kutoa maamuzi yaliyowagusa wakazi wa eneo hilo na wanakigoma kwa ujumla.
‘’Nawaagiza wataalam watakaohusika na utoaji wa vibali kwa ajili ya uendelezaji wa makazi katika eneno hili kuhakikisha wanatekeleza zoezi hili kwa uadilifu mkubwa na utoaji wa vibali usizidi siku Thelathini tangu siku ya kupokea maombi ya vibali hivyo.’’ Amesema Andengenye.
Amesisitiza kuwa wananchi watakaokutana na kadhia yoyote wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, wasisite kutoa taarifa kwa uongozi wa juu ili kuchukua hatua kwa yeyote atakayeonekana kukwamisha utendaji kazi.
Baadhi ya Wananchi wenye majengo pamoja na viwanja katika eneo hilo, hawakusita kumshukuru Waziri Jafo pamoja na Uongozi wa Mkoa kwa kufikia maamuzi hayo yenye tija kwao na Jamii ya wanakigoma kwa ujumla.
‘’Sula hili limeleta sintofahamu kwetu kwa zaidi ya miaka kumi na tatu, hivyo maamuzi yaliyofikiwa yametugusa na kutufanya tuwe na Amani kwa sababu baadhi yetu walilazimika kuishi katika nyumba za kupanga wakati wakisubiri hatma ya suala hili’’ alisema Rajabu Maboza Mkazi wa kata ya Sanganigwa Manispaa ya Kigoma-Ujiji.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa