NA. GRADNESS KUSAGA-KIGOMA
Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imedhamiria kutekeleza mpango wa kudumu wa usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa bure ili kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anapata haki hiyo.
Akizungumza kwenye Hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye Umri chini ya miaka mitano mkoani Kigoma iliyofanyika katika viwanja vya Mwanga Centre, Waziri Dkt. Chana amesema cheti cha kuzaliwa ni haki ya Msingi kwa kila mtoto anayezaliwa ndani ya mipaka ya Tanzania.
Amesema Serikali imeandaa mpango huo ikilenga kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa vyeti hivyo, inayotolewa karibu na makazi ya wananchi kupitia Ofisi za watedaji wa kata na vituo vya kutolea Huduma za Afya vilivyopo katika maeneo yao ili kuwapunguzia upotevu wa muda na fedha kwa ajili ya kufuata huduma hiyo katika makao makuu ya wilaya.
Amefafanua kuwa, Tangu kuzinduliwa kwa mpango huo Juni 2023, zaidi ya watoto Mil. 8.6 wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa katika mikoa 24 ambayo mpango huo unaendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wake.
‘’Niendelee kuwakumbusha kinamama wajawazito kujifungua kwenye vituo vya Afya ili mtoto anapozaliwa aweze kupata cheti chake cha kuzaliwa na mzazi unapaswa kukichukua kwa kuwa ni haki ya mtoto aliyezaliwa’’ amesisitiza Dkt. Chana.
Aidha mpango huo mkoani Kigoma unawalenga jumla ya watoto 393,216 wenye umri chini ya Miaka mitano ambao wanatarajiwa kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa wilaya ya Kigoma Salum Kalli amesema mkoa unajumla ya vituo 443 kwa ajili ya ya kutolea huduma ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa.
Amesema kuwa wataalam watakaohusika na utekelezaji na usimamizi wa zoezi hilo wamejipanga kukabiliana na changamoto za uwepo wa Raia wa nchi jirani kwa kubainisha uhalisia wa taarifa zao.
Pia Kalli amewakumbusha wazazi wajibu wa kutunza vyeti hivyo kwa kuwa ni kumbukumbu muhimu za maisha ya watoto wao ili waweze kuwakabidhi pale watakapofikia umri wa kutosha kutambua umuhimu wa nyaraka hizo.
Upande wake Mwakilishi wa Serikali ya Canada ambao ni wafadhili wa mpango huo Bronwin Crude amesema nchi yake inajivunia kuunga mkono utekelezaji wa mpango huo kwa sababu usajili wa vizazi ni haki ya msingi kwa ajili ya kupanga mipango ya Maendelo ya nchi.
Aidha amesisitiza kuwa mfumo wa usajili wa vizazi unazingatia jinsia zote ili kuhakikisha haki za watoto zinalindwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa katika Siku zijazo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa