Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewasili mkoani Kigoma na kupokelewa na Katibu Tawala Mkoa Albert Msovela kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, ambapo anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye Hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa Usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya Umri wa miaka mitano mkoani hapa itakayofanyika Oktoba 3, 2023.
Akizungumza kwenye kikao kifupi cha kupokea Taarifa ya Maandalizi ya Uzinduzi huo, Waziri Dkt. Chana ameupongeza Uongozi wa mkoa kwa kufanikiwa kuendesha mchakato wa ushirikishaji Jamii kwa kuhusisha wadau na makundi mbalimbali kwa lengo la kutoa Elimu na kufikisha ujumbe uliolenga kufanikisha zoezi hilo mkoani hapa.
Waziri huyo amesisitiza kuwa, watendaji wa Serikali wanatakiwa kutanguliza weledi, uzalendo na umakini mkubwa katika kutekeleza zoezi hilo kutokana na baadhi ya wakazi wa nchi jirani kutumia fursa hiyo kama kigezo cha kuwapatia watoto wao uraia wa Tanzania.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Programu hiyo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Lebba amesema kuelekea uzinduzi huo vimefanyika vikao mbalimbali na uongozi wa RITA, Timu za Wataalam wa Mkoa, Kamati za Usalama Mkoa na Wilaya, Idara ya wakimbizi, Maafisa Ustawi wa Jamii mkoa na Halmashauri kwa lengo la kuwajengea uelewa pamoja namna bora ya kutekeleza majukumu yao kuhusiana na zoezi hilo.
Amefafanua kuwa, Mkoa umefanikiwa kutoa mafunzo kwa ajili ya wasaidizi kutoka ngazi za kata pamoja na vituo vya kutolea Huduma za Afya ambapo Jumla ya wasaidizi 544 wamefikiwa kwa lengo la kupatiwa maarifa ya utekelezaji wa zoezi.
Amesisitiza kuwa, katika kuhakikisha wanaifikia Jamii wameendelea kutumia vyombo vya Habari, mitandao ya kijamii, watu maarufu, taasisi za Umma pamoja na maeneo ya mikusanyika ya watu kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa walengwa.
Hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya Miaka mitano kimkoa itafanyika katika Uwanja wa Community Centre uliopo Kata ya Mwanga Manispaa ya Kigoma Ujiji.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa