Baadhi ya wadau waliojitokeza kwenye Hafla fupi ya uzinduzi wa vitabu vya Miongozo ya Uboreshaji wa Elimu nchini uliofanyika katika Ukumbi wa NSSF-Kigoma.Utepe ukikatwa kuashiria uzinduzi wa vitabu vya Miongozo ya Uboreshaji wa Elimu nchini kwa Mkoa wa Kigoma.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amewataka wazazi na walezi kushirikiana na walimu ili kutokomeza changamoto ya Utoro sugu mashuleni na kuimarisha maendeleo ya Elimu mkoani hapa.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo kwenye hafla fupi ya uzinduzi wa vitabu vya Miongozo ya Uboreshaji wa Elimu nchini, iliyofanyika katika Ukumbi wa NSSF Manispaa ya Mji Kigoma-Ujiji, mkoani hapa, vikiwa na lengo la kuboresha elimu kwa ngazi za Msingi na Sekondari.
Alisema wazazi waachane na dhana yakuwategemea walimu pekee katika kusimamia na kufuatilia mahudhurio pamoja na maendeleo ya wanafunzi kwa lengo la kudhibiti utoro na kuboresha maendeleo ya wanafuzi kitaaluma.
Andengenye alisema, ili kufanikisha mikakati mbalimbali ya maendeleo ya Elimu mkoani hapa, Jamii haina budi kushirikiana na Wataalam wa Idara ya Elimu kwa ngazi mbalimbali ili kufikia malengo ya kuinua Taaluma yanayondelea kuwekwa na Serikali.
‘‘Tumebaini kutoongezeka kwa ubora wa ufaulu katika Mkoa ambapo kupitia Mtihani wa Ukamilifu kwa Darasa la Saba uliofanyika mwezi Septemba 2022 ufaulu ulikuwa ni asilimia 47, huku upande wa Sekondari waliofaulu kwa Daraja la I hadi la III ikiwa ni Asilimia 29, Daraja la IV Asilimia 45, huku waliofeli kabisa ikiwa ni Asilimia 27’’ alisema.
Naye Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Kigoma David Mwamalasi, alisema watendaji wanapaswa kuisimamia kwa ukamilifu na uadilifu miongozo hiyo ili iweze kuleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa na Serikali ili kuboresha Elimu katika mkoa huo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Muhambwe Dkt. Frorence Samizi, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa Fedha kwa ajili ya kugharimia miradi mbalimbali ya Elimu katika Jimbo lake pamoja na Mkoa wa Kigoma kwa ujumla.
Tutaendelea kushirikiana na walimu ili kuhakikisha malengo yanayowekwa na Serikali katika uboreshaji wa elimu yanafanikiwa'' alisema.
Miongozo mitatu iliyozinduliwa mkoani hapa ni Mwongozo Mkakati wa Kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji Ngazi ya Elimu Msingi, Mwongozo wa kubainisha Changamoto katika uboreshaji Elimu Msingi na Sekondari, Mwongozo wa Uteuzi wa Viongozi wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa