WATUMISIHI WA AFYA MKOANI KIGOMA WATAKIWA KUFUATA MAADILI YA KAZI
Posted on: May 12th, 2017
Watumishi wa sekta ya Afya wametakiwa kuwa na nidhamu ya kazi na kuzingatia maadili ya tasnia yao wanapokuwa katika kutekeleza majukumu yao ikiwa pamoja na matumizi ya lugha nzuri, kuheshimiana na kuthaminiana.
Haya yameelezwa wakati wa ziara na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wa Kigoma, Mhe. Brigedia Jenerali (mstaafu) Emanuel Maganga alipokuwa anazungumza na watumishi wa Hospitali ya Mkoa ya Rufaa –Maweni Mkoani Kigoma.
Alisema kuwa ili kuwa na maendeleo suala la afya za watu ni lazima lipewe umakini mkubwa, hii ni pamoja na kwanza watumishi kushirikiana wao kwa wao pamoja na wanaowahudumia “wasaidieni wananchi waeleimisheni pia masuala ya lishe kuepukana na udumavu pamoja na unyafuzi”.
Mhe. Maganga amewapongeza na kuwashukuru Wafanyakazi wote wa Hospitali ya Rufaa ya Maweni kwa kuwatumikia watanzania katika suala zima la afya. Ameendelea kuwahimiaza wachape kazi, licha ya changamoto wanazozikabili Serikali ya awamu ya tano inatambua hayo na inayafanyia kazi yatakwisha kwa awamu.
Akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Afya Dkt Paul Chaote alieleza kuwa pamoja na kuwepo kwa Changamoto hospitali imejitahidi kuongeza ukusanyaji wa mapato kupitia fedha za uchangishaji (cost sharing) ambapo makusanyo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki yameimarika kutoka milioni 23,541,700 mwezi Julai 2016 hadi Shilingi Milioni 32,049,340 mwezi Machi 2017.
Dkt. Chaote ametaja pia upugufu wa watumishi ni changamoto inayoikabili. Hospitali inaupungufu wa watumishi 451 kati ya 681 wanaohitajika, alieleza kuwa kati ya mapungufu hayo kuna mapungufu ya Madaktari bingwa hali ambayo inachangia rufaa nyingi kutolewa ambazo zingeweza kufanyika haospitalini hapo. Hata hivyo ameishukuru Serikali kwani imeanza kuleta watumishi katika hospitali hiyo ambapo hivi karibuni wameripoti madaktari watatu.