Watumishi wa Umma katika halmashauri za Mkoa wa Kigoma wametakiwa kuzingatia kanuni, taratibu na Sheria za matumizi ya Fedha za Umma ili kuepuka kusababisha hoja za ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika Halmashauri hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza na Madiwani kupitia Mikutano Maalum wa mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri Wilaya ya Kigoma na Manispaa ya Kigoma Ujiji, kwa ajili ya kujadili hoja na Mapendekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 uliofanyika Juni 21. 2024 katika Halmashauri hizo.
‘‘Ili kudhibiti hoja katika maeneo yenu mnatakiwa kuwasilisha nyaraka za matumizi yote ya fedha kwa wakati sambamba na kutoa ushirikiano wa karibu kwa wakaguzi wa ndani katika Halmashauri zenu’’ amesisitiza Andengenye.
Amesema lengo la mkoa ni kuhakikisha halmashauri zote ziwe zinashughulikia hoja zisizozidi tisa ifikapo mwaka 2025/2026 kutokana na mkoa kuanza kutekeleza mkakati wa kubaini na kudhibiti viashiria kabla havijawa hoja kamili.
Aidha amezitaka halmashauri hizo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya ndani sambamba na kutumia Asilimia Arobaini ya Mapato hayo kutekeleza miradi inayoonekana na kuwagusa wananchi moja kwa moja badala ya utekelezaji wa miradi ya kwenye makaratasi.
Sambamba na hilo, mkuu huyo wa mkoa amezielekeza halmashauri hizo kuhakikisha zinapima maeneo yote yanayomilikiwa na Taasisi za Umma na kuzipatia hati miliki ili kudhibiti wavamizi wanaosababisha ongezeko la kesi za migogoro ya ardhi.
Aidha Mkuu wa mkoa ametoa wito kwa wakazi mkoani hapa kujitokeza na kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lililolenga kutoa fursa ya kuandikisha wapiga kura wapya, kurekebisha taarifa za wapiga kura sambamba na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika orodha hiyo.
Upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa amesema mkoa umejipanga kuongeza ushirikiano na wakaguzi wa ndani ili kupunguza idadi ya hoja hadi kufikia chini ya kumi kwa kila halmashauri kwa kila mwaka wa fedha.
Aidha amewaelekeza wakurugenzi kuhakikisha wanawasimamia wakuu wa Idara na Vitengo ili waweze kujibu hoja zinazojitokeza kwa usahihi na kuzingatia muda kwa sababu majibu ya hoja hizo yapo chini ya mamlaka yao.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala amewataka madiwani hao kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha uchangiaji wa chakula shuleni ili wanafunzi waweze kupata chakula shuleni kwa lengo la kudhibiti mdondoko wa wanafunzi katika baadhi ya shule za Halmashauri mkoani hapa.
Kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na wilaya ya Kigoma vijijini zimefanikiwa kupata hati safi ya ukaguzi wa Hesabu za Serikali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa