Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka watumishi wa Umma mkoani hapa kuendelea kushirikiana ili kuleta matokeo chanya katika utendaji kazi wao kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Andengenye ametoa wito huo alipozungumza na watumishi katika Halmashauri ya Buhigwe aliposhiriki hafla fupi ya kuwapongeza wafanayakazi hodari kwa mwaka 2023/2024 waliotambuliwa na Halmashauri hiyo kupitia maadhimisho ya Mei Mosi 2024 yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Amewaeleza watumishi hao kuwa, ni vizuri kila mmoja akatambua na kutekeleza wajibu wake kuendana na miongozo ya kazi yake badala ya kusubiri kusukumwa na viongozi wake katika eneo la utendaji kazi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi wa watumishi wa Umma mkoani hapa kujenga tabia ya kutumia njia ya hamasa ili kuwapa motisha chanya watumishi hao badala ya kutumia lugha za vitisho, jambo linalosababisha kushuka kwa ari ya utendaji kazi.
‘‘watu wakikosa ari ya kufanya kazi hujikuta wakihudhuria ofisini badala ya kufima maeneo hayo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao, kutoakana na hofu ya kuachishwa kazi au vitisho kutoka kwa wasimamizi wao, jambo hili ni changamoto kubwa katika ofisi zetu’’ amesema Andengenye.
Kiongozi huyo amewataka watumishi mkoani hapa hususani waliopo katika Wilaya ya Buhigwe kutumia fursa ya uwepo wa rasilimali ardhi katika halmashauri hiyo kwa lengo la kuwekeza katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ili kujiimarisha kiuchumi.
Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Ngayalina amewakumbusha watumishi hao kuendelea kuitumikia jamii ili waweze kuacha alama.
Aidha amewapongeza watumishi wote wa halmshauri hiyo kwa umoja walionao katika utekelezaji wa majukumu yao huku akiwataka kuongeza bidi katika utendaji kazi na kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi na kuwaondolea kero zao.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo George Mbilinyi amesema kitendo cha kuwatambua watumishi hodari na kutoa pongezi katika hamashauri kinatoa motisha na chachu kwa watendaji wengine kuongeza bidi katika utendaji kazi wao ili kuyafikia malengo yaliyowekwa na kuwapa fursa ya kutambuliwa katika wakati ujao.
‘’Niwaombe watumishi wenzangu tuzidi kufanya kazi ili tuiletee wilaya ya Buhigwe matokeo ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anayatarajia tuyafikie katika kutatua changamoto za wakazi’’ amesisitiza Mbilinyi.
PICHA ZA PAMOJA ZA WASHIRKI WAKIWA NA MGENI RASMI MHE. KAMISHNA MSTAAFU WA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI THOBIAS ANDENGENYE.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255738192977
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa