Watu 40,000 kupata chanjo ya UVIKO 19 Mkoani Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 leo tarehe 03 Agosti 2021 katika kituo cha kutolea chanjo kilichopo katika Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Maweni iliyopo katika manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akizindua zoaezi la utoaji chanjo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amesema katika awamu ya kwanza chanjo inatarajiwa kutolewa kwa watu 1,708 katika vituo 24 vilivyopo katika almshauri za Mkoa wa Kigoma ambapo wananchi waliotayari kuchanjwa watajisajili katika mfumo wa Taifa wa Chanjo ama katika vituo vilivyo chaguliwa katika Halmashauri husika na watapatiwa cheti baada ya kuchanjwa.
Uzinduzi wa chanjo hii katika Mkoa wetu wa Kigoma, unatoa fursa kwa Wananchi ambao wako tayari kuchanjwa kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa pamoja na kupunguza hatari ya kupata ugonjwa na madhara makubwa endapo mtu atapata maambukizi. Amesema Andengenye.
Amesema zoezi la kuchanja litafuata Mwongozo wa Chanjo wa Taifa dhidi ya Ugonjwa wa UVIKO-19, Shirika la Afya Duniani (WHO), ambapo amebainisha kuwa chanjo hizi kwa sasa zinatolewa kwa kufuata vipaumbele vya makundi yenye uhitaji mkubwa ambayo Watumishi wa sekta ya Afya, watu wazima wenye umri wa miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa sugu, amesisitiza kuwa uchanjaji kwa makundi yote ni wa hiari au huru kwa kila mwananchi
Andengenye ametoa onyo kwa taasisi itakayotoza gharama ya aina yoyote katika utoaji wa chanjo hiyo ambayo ni bure kwa kila mhitaji alisema ānaelekeza kwa huu mgao wa COVAX FACILITY ni marufuku Hospitali yoyote (ya umma au binafsi) kulipisha Wananchi gharama yoyote katika zoezi hili la chanjo na lifanyike kwa uadilifu na kwa haki kwa walengwa wa sasa
Andengenye ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, kufanikisha upatikanaji wa chanjo hii hapa nchini pia ameendelea kuwasisitiza Wananchi kuendelea kujikinga na UVIKO-19 kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali za mita moja au zaidi, kuepuka misongamano na kufanya mazoezi.
Amewataka Wanahabari, Wananchi, Viongozi wa Jamii, Viongozi wa madhehebu ya Kidini na wengineo kuhakikisha wanapeleka ujumbe kwa jamii kuhusu huduma za chanjo, kuwaelimisha na kuwaelekeza Wanachi kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili wapate chanjo.
Kwani Jamii ya Kigoma ikiwa imekingwa itapunguza milipuko ya mara kwa mara ambayo husababisha magonjwa na vifo. Vilevile jamii ikichanjwa itadumisha kiwango cha juu cha chanjo na hivyo kuboresha uchumi na maisha kwa ujumla alisema Mkuu wa Mkoa.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya usambazaji wa chanjo za UVIKO-19 katika Mikoa kumi iliyoripotiwa kuwa na maambukizi mengi ya Ugonjwa wa UVIKO 19 hapa nchini ukiwemo Mkoa wa Kigoma ambapo chanjo aina ya Janssen kutoka Kampuni ya Johnson & Johnson ya nchini Marekani ndiyo inayotolewa..
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
HakimilikiĀ©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa