KATIBU TAWALA MKOA WA KIGOMA ALBERT MSOVELA AKITOA TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI (HAWAPO PICHANI) KUHUSU ZOEZI LA UTOAJI WA KINGATIBA KWA AJILI YA KUDHIBITI MAGONJWA YA MINYOO YA TUMBO NA KICHOCHO MKOANI KIGOMA.
MRATIBU WA MAGONJWA YASIYOPEWA KIPAUMBELE MKOA WA KIGOMA INNOCENT MSILIKALE AKISHIRIKI KATIKA MKUTANO WA KATIBU TAWALA NA WAANDISHI WA HABARI ULIOLENGA KUTOA TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEKELEZAJI WA ZOEZI LA UTOAJI WA KINGATIBA MKOANI KIGOMA.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI inaendesha zoezi la umezeshaji vidonge vya Kingatiba kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya Minyoo ya tumbo na Kichocho kwa watoto kuanzia umri wa miaka mitano hadi 14 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi ikiwemo mkoa wa Kigoma.
Akitoa Taarifa kwa Umma kuhusu uendeshaji wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amesema mkoa umepokea jumla ya vidonge 793,000 aina ya Plaziquantel na 548,200 aina ya Albendazole kwa lengo la kuchanja watoto 505,840 walioko ndani nan je wa utaratibu wa shule.
Amesema Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele, imedhamiria kutekeleza mpango huo ili kuhakikisha watanzania wanakuwa na Afya Bora kwa kuwakinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Amesisitiza kuwa, ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa, Jamii inapaswa kutoa ushirikiano kwa wataalam wa Afya katika kuwatambua walengwa na kuhakikisha wanafikiwa kisha kupatiwa huduma.
‘’Nitoe wito kwa wadau mbalimbali wa Afya na Jamii kwa ujumla kuhakikisha tunashirikiana na srikali katika utekelezaji wa zoezi hili ili walengwa wote waweze kufikiwa, aidha Jamii ikumbuke wajibu wake wa kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo kuendana na miongozo ya wizara ya Afya’’ amesisitiza Msovela.
Akitoa taarifa ya Maendeleo ya utekelezaji wa zoezi hilo Mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele mkoa wa Kigoma, Innocent Msilikale amesema utekelezaji wa zoezi hilo umekuwa ukikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo uelewa duni wa wakazi kuhusu umuhimu wa zoezi hilo pamoja na hofu itokanayo na uwepo wa maudhi madogo madogo yatokanayo na matumizi ya dawa hizo.
Aidha Msilikale amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, elimu kuhusu umuhimu wa kingatiba hizo inaendelea kutolewa kwa wazazi, walimu na jamii kwa ujumla sambamba na kuhamasisha ulaji shuleni wakati wa utoaji wa dawa hizo
Zoezi la ugawaji kingatiba ya magonjwa ya minyoo na kichocho limeanza kutekelezwa kuanzia tarehe 13 hadi 24, Novemba 2023 likihusisha Halmashauri nane za mkoa wa Kigoma.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa