MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE(KUSHOTO) AKIMTWISHA NDOO YA MAJI MKAZI WA KIJIJI CHA BIHARU (JINA HALIKUPATIKANA) MARA BAADA YA KUTEMBELEA KISIMA KILICHOFANYIWA MABORESHO KUPITIA MRADI WA TASAF KATIKA KIJIJI HICHO.
Watendaji wa serikali mkoani Kigoma wametakiwa kuongeza ubunifu katika kuibua changamoto zinazowakabili wananchi kisha kutumia fedha zinazotolewa na serikali pamoja na rasilimali mbali mbali zilizopo katika jamii kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yao ya utendaji kazi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza na wakazi katika kijiji cha Biharu alipokuwa akikagua utekelezaji wa miradi chini ya mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Buhigwe na kusisitiza kuwa, watendaji wa Serikali wanatakiwa kutekeleza majukumu kwa kiwango kitakacho acha alama kwa wananchi wanaowahudumia.
Amesema wataalam wanatakiwa kushirikiana kwa ukaribu na wananchi ili waweze kuibua changamoto zao hususani katika upatikanaji wa huduma za kijamii na kutumia vizuri rasilimali zilizopo ili kuwaondolea kero wakazi mkoani humo.
Kupitia fedha inayoekekezwa kwa walengwa hao kwa lengo la kutekeleza miradi ya kijamii katika kijiji cha Biharu, mradi umefanikiwa kuboresha vyanzo vitatu vya Maji kwa kuvijengea pamoja na kusafisha mazingira yanayovizunguuka ili kuhakikisha wakazi wanapata maji safi.
Aidha katika kijiji hicho shughuli nyingine zinazotekelezwa na walengwa hao ni pamoja na kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa, ufugaji sambamba na Kilimo cha mazao ya chakula.
Felesia Issaya mkazi wa kijiji cha Biharu ambaye pia ni mnufaika wa mradi huo, anasema uboreshaji wa vyanzo vya maji katika vitongoji vya Kaguruka, Kagunga na lulema vilivyopo kijijini hapo umewaondolea changamoto ya kuwaepusha kutumia maji pamoja na mifugo.
‘’Kwa sasa kila chanzo kimewekewa barabara ya kuingilia kwa watumiaji, uwekaji wa bomba la kutolea maji kwenye visima pamoja na utunzaji wa mazingira katika maeneo ya vyanzo’’ amesema Felisia.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa