Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewasisitiza watendaji wa Serikali mkoani hapa kuongeza kasi katika kufuatilia na kusimamia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ili ziweze kutumika ilivyokusudiwa katika kuwaletea wananchi Maendeleo wananchi.
Maelekezo hayo ameyatoa leo Januari 20, 2024 alipozungumza wakati akifungua kikao cha Kuwasilisha na kufanya Uchambuzi wa Bajeti ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma.
Aidha kiongozi huyo wa Mkoa amewakumbusha watendaji hao kuongeza ushirikiano katika utendaji kazi wao jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi na kurahisisha jukumu la kutoa huduma kwa wananchi ili kuongeza kasi ya Maendeleo ya Mkoa.
Viongozi, mojawapo ya jukumu lenu ni kuhakikisha watendaji walio chini yenu mnawajengea uwezo ili waweze kujiamini na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi’’ amesema Andengenye.
Kupitia kikao hicho Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu kwa kuendelea kuelekeza kiasi kikubwa cha Fedha mkoani hapa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo jambo linaloendelea kuthibitisha dhamira yake katika kuufungua mkoa na kuufanya kuwa kitovu cha kiuchumi katika ukanda wa magharibi.
Upande wake katibu Tawala mkoa wa Kigoma Albert Msovela amewasisitiza watendaji hao kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu hatua mbalimbali zinazofikiwa katika kazi za utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
‘’Niwasisitize kutoa taarifa za kila hatua mnayofikia katika utekelezaji wa kazi za miradi ya maendeleo, hii itasaidia kupata ushauri na kuondoa mikwamo kwa haraka kabla haijaathiri utendaji mzima wa kazi’’ amesema Msovela.
Kikao hicho kimehudhuriwa na wakuu wa wilaya, wakuu wa Idara na Sehemu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, makatibu Tawala (w), wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na maafisa mipango wa Halmashauri nane za Mkoa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa