Wataalam 44 kutoka katika Idara na Vitengo vya Halmashauri nane za Mkoa wa Kigoma wametakiwa kutumia ujuzi walioupata kupitia mafunzo ya Mfumo mpya wa Ununuzi Serikalini (NeST) kwenda kudhibiti manunuzi holela yanayosababisha uwepo kwa mianya ya rushwa na ubadhilifu wa Fedha katika maeneo ya kiutumishi.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Frank Makua ametoa Kauli hiyo wakati akifunga mafunzo hayo na kusisitiza kuwa, ufanisi wao utasaidia kuzuia Serikali kupata hasara na kuimarisha utoaji wa Huduma bora kwa Umma.
Makua amesema Serikali ilibaini dosari mbalimbali katika kusimamia mifumo na taratibu za ununuzi katika Sekta za Umma, jambo lililochangia kutopatikana kwa usawa na utimilifu katika utoaji huduma zinazoendana na Thamani ya Fedha inayotolewa.
‘’Nasisitiza mtumie mafunzo haya katika kulinda ubora wa Huduma zinazotakiwa kutolewa na Serikali kwa Wananchi, hivyo mkawe walimu na mabalozi wazuri katika matumizi ya mfumo huu’’ amesisitiza’’
‘’Tumepokea zaidi ya Bil. 19 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2023/2024, niwasisitize kuwa, fedha zote zinazotakiwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo zipitie Mfumo wa NeST kama ilivyoagizwa na Serikali’’ ameendelea kusisitiza Makua.
Upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Mkoa Ashura Sadick amesema wakuu hao wa Idara na Vitengo wanapaswa kushirikiana na wazabuni ili kujenga mazingira rafiki ya kufanikisha matumizi ya mfumo huo wa manunuzi.
Aidha, Ashura amesisitiza kuwa Kitengo chake kitakuwa Tayari nyakati zote kutoa msaada wa kitaalam ili utendaji kazi wa mfumo uweze kutoa huduma nyakati zote ili kuwaepushia watoa huduma na wapokeaji kutokwama kufikia malengo yao.
Kadhalika baadhi ya wataalam hao kutoka Halmashauri wameonesha kuelewa na kuridhishwa na utaratibu uliotumika kutoa mafunzo hayo, huku wakisistiza uwepo wa mawasiliano ya karibu baina ya wasimamizi wa mfumo ili zinapotokea changamoto ndogondogo ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati na kutozorotesha utoaji wa Huduma kwa wananchi.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa