Wataalam wa Timu za Utekelezaji wa Mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi ‘’BOOST’’ Kanda ya Magharibi wameshiriki mafunzo elekezi kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa utekelezaji wa Mradi huo, yaliyofanyika Leo Desemba katika Chuo cha Ualimu Kasulu Mkoani hapa.
Awali akifungua Mafunzo hayo, Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Kigoma Bi. Paulina Ndigeza amewasisitiza washiriki kuwa, mara baada ya mafunzo hayo wakatekeleze wajibu wao kwa uthabiti ili kupata matokeo chanya katika Sekta ya Elimu kama ambavyo Serikali inavyotarajia.
‘‘Tutumie nafasi hii kujifunza kwa bidii na tuhakikishe tunaelewa dhamira ya Mradi huu kwa kuwa malengo ya Serikali na Wahisani ni kuhakikisha tunafanya maboresho makubwa katika mfumo wa Elimu nchini ikiwemo kuongeza udahili wa Elimu awali pamoja na kujenga Mazingira rafiki ya ujifunzaji na ufundishaji’’ amesema Ndigeza.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kiasi kikubwa cha Fedha katika kuimarisha Miundombinu ya Elimu pamoja na kuchukua hatua za kuwezesha utekelezaji wa kazi mbalimbali za kielimu nchini.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo Bi. Joyce Mushi kutoka OR-TAMISEMI, Amesema Mradi huo wa BOOST wenye thamani ya Shilingi Tril. 1.15 ambazo ni ufadhili kutoka Benki ya Dunia, umelenga kuzifikia Shule 6000 na kuwafikia zaidi ya watoto Milioni 12 nchini.
Amewasisitza wanamafunzo kutanguliza uzalendo ili kufikia malengo jambo litakalotoa fursa ya kuendelea kuaminiwa na kupata mikopo zaidi ili kubotresha na kuimarisha Sekta ya Elimu.
‘‘Kama ambavyo tunaendelea kuwaelekeza, hakikisheni mnaenda kufanya kazi kuendana na Miongozo na Mafundisho tunayowapatia, hii itatoa fursa ya kuendelea kupata misaada zaidi ambayo itatoa nafasi ya kuwagusa watu wengine kwani mahitaji yetu katika kuiimarisha sekta ya Taaluma ni makubwa sana’’
Mafunzo hayo ya Siku mbili yanaratibiwa na kutekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya OR-TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Fedha ambapo washiriki wanajengewa uwezo katika Afua za Uboreshaji wa Miundombinu, Uwekaji Mazingira Salama ya Ufundishaji na Ujifunzaji, kuongeza udahili wa Wanafunzi wa Elimu awali, Uboreshaji mazingira ya kielimu, utoaji mafunzo endelevu kwa walimu kazini, kuwezesha upatikanaji wa Rasilimali za utoaji Huduma katika Halmashauri.
Timu za utekelezaji wa Mafunzo hayo, zinaundwa na wakuu wa Idara na Vitengo vya Elimu Msingi, Manunuzi, Maendeleo ya Jamii, Uthibiti Ubora wa Elimu, Walimu ngazi ya Shule za Msingi, Wahandisi, Maafisa Habari pamoja na Mratibu wa Mradi ngazi ya Mkoa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa