Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye ametoa wito kwa Wakazi kujitokeza na kuwasilisha malalamiko yao kwenye Kamati ya maadili ya Mkoa ikiwa ni pamoja na matukio ya rushwa, ubaguzi na vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa maadili vinavyofanywa na maafisa wa Mahakama mkoani Kigoma.
Kamati hiyo inayojumuisha wadau kutoka ngazi za Serikali, Mahakama na Jamii imeundwa na hutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya 2011, Kifungu cha 50(1) ikiwa na lengo la kuhakikisha maafisa wa mahakama wanazingatia maadili katika utendaji kazi.
Mkuu wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, amesema malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa maandishi au wahusika kufika wenyewe kwenye Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa kisha yatafikishwa kwenye Kamati ya uchunguzi na kutolewa maamuzi kutokana na uthibitisho utakaopatikana.
Nae, mjumbe wa Kamati hiyo na Afisa Sheria katika Sekretarieti ya Mkoa wa Kigoma Diana Joseph, amesema Kamati hiyo hutoa mapendekezo kutokana na uthibitisho wa taarifa za malalamiko zinazowafikia kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha maadili ya kiutumishi yanafuatwa kwa maslahi ya Taifa.
Kamati ya maadili ya Maafisa wa Mahakama hukutana kila robo Mwaka ambapo wajumbe hupitia malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi mkoani Kigoma kisha kutoa mapendekezo kwenye Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa ajili ya hatua zaidi za Kisheria iwapo itathibitika ukiukwaji wa maadili kwa watumishi husika.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa