Wanufaika wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Kigoma wametakiwa kujiunga na vikundi vya wajasiriamali ili kupata fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo mikopo yenye riba nafuu kutoka kwenye taasisi rasmi zinazotambulika kiserikali.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alipozungumza na wanufaika wa mpango huo mara baada ya kufunga Kikao kazi cha Viongozi wa Mkoa na Wilaya kilichofanyika mjini Kasulu kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi kwa kipindi cha 2023/2024 na kuwasisitiza wanufaika umuhimu wa kutumia fedha wanazopata kuendana na malengo ya serikali ikiwemo kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Amesema suala la kuitwa masikini sio sifa hivyo inapopatikana fursa ya kujikwamua kiuchumi na kujitoa katika kundi hilo, wananchi wanapaswa kuchangamkia nafasi hizo ili wwaweze kumudu kuendesha maisha yao bila utegemezi wa misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali pamoja na Serikali.
''Tumepata shuhuda mbalimbali pamoja na kujionea namna ambavyo mpango huu umefanikiwa kubadili maisha ya wanufaika ikiwemo kununua mashamba, kujenga makazi bora, kuongeza tija kwenye kilimo, kusomesha, kuanzisha na kuimarisha biashara pamoja na kutatua changamoto za kifamilia ikiwemo uhakikika wa upatikanaji wa chakula na matibabu'' amesema Andengenye.
Aidha Andengenye amewasisitiza wanufaika kutumia fedha wananyoipata kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shuleni, wanapata matibabu kwa wakati, wanapata lishe bora pamoja na kuwakinga na maradhi ili waweze kuwa timamu kimwili na kiakili.
David Mzirai ambaye ni Afisa Ufuatiliaji Mradi wa TASAF kwa wilaya ya Kigoma amesema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wanufaika kutofuzu pamoja na kufikia malengo au sifa zinazostahili, jambo linalonyima fursa kwa wahitaji wengine kufikiwa na huduma hiyo.
Aidha amesisitiza kuimarishwa kwa mikakati itakayosaidia kuondoa wimbi la wanufaika wasio na sifa ili kutoa fursa kwa wahitaji wenye sifa kupata huduma hiyo kama ilivyokusudiwa na serikali
Mzirai ameahidi kuendelea kushirikiana na uongozi unaosimamia mradi ili kudhibiti watu wasio na sifa kuendelea kunufaika sambamba na kuwahamasisha wenye sifa kuhudhuria kwenye warssha za kijamii ili kuwajengea uwezo kimatumizi.
Upande wake Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma CPA Johnson Gamba ameshauri Serikali kupitia waratibu wa Mpango huo kuweka muda rasmi wa ukomo kwa wanufaika ili kutoa fursa kwa watanzania wengine wenye uhitaji kufikiwa na huduma hiyo.
Wakitoa ushuhuda wa manufaa waliyoyapata kupitia mradi huo, Cesilia Richard amesema kupitia mradi huo, ameweza kujenga nyumba ya vyumba viwili, kusomesha watoto pamoja na kuimarisha biashara anayoifanya.
Amesema kupitia mradi wa TASAF amefanikiwa kupata mtaji unaomfanya aweze kuendesha maisha yake na familia kwa ujumla na kumpunguzia adha ya kutegemea ndugu na jamaa.
Kupitia ushuhuda huo walioutoa mbele ya Mkuu wa Mkoa, Bi Leonia Hwaga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia kwa kuufanya mradi huo kuwa endelevu ambapo amefanikiwa kuanzisha ufugaji, amenunua mashamba mawili pamoja na kusomesha watoto wawili.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa