WANUFAIKA WA MRADI WA TASAF MTAA WA MWINYI MJINI KASULU WAKIKABIDHI ZAWADI YA MBUZI KWA MKUU WA MKOA WA KIGOMA THOBIAS ANDENGENYE ALIPOFANYA ZIARA WILAYANI HUMO KWA LENGO LA KUKAGUA MAENDELEO YA UTEKELEZAJI WA MRADI HUO.
Wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) mkoani Kigoma wametakiwa kutumia fedha wanazozipata kutokana na mradi huo kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa ili waweze kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Wilaya za Buhigwe, Kasulu na Uvinza, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amesema njia pekee ya kunufaika na fedha hizo ni kuunganisha nguvu miongoni mwao na kuanzisha miradi midogo midogo ili waweze kuzalisha kupitia kiasi cha fedha wanachopokea na kutimiza malengo wanayojiwekea.
WANUFAIKA WA MRADI WA TASAF MTAA WA MWINYI MJINI KASULU WAKIFUATILIA UTOAJI TAARIFA YA MRADI WA SHAMBA LAO LA MITI KWA MKUU WA MKOA WA KIGOMA.
Andengenye amewakumbusha wanufaika wa mradi huo kujikita katika shughuli za uzalishaji ambazo hazitohitaji gharama kubwa kiuendeshaji na kuwawezesha kupata kipato kitakachokidhi mahitaji yao.
Amesema lengo la Serikali kupitia mradi huo ni kuhakikisha watanzania wenye kipato kidogo wanaweza kumudu gharama za maisha ikiwemo kupata matibabu, chakula, makazi, mitaji midogo ya Biashara sambamba na kuwezesha gharama za manunuzi ya mahitaji ya shule kwa wanafunzi kutoka kaya hizo.
ENEO LA SHAMBA LA KIKUNDI CHA WANUFAIKA WA TASAF KATA YA MWINYI LENYE MITI 900 AINA YA PINUS. SHAMBA HILI AWALI LILIKUWA ENEO LA KUHIFADHIA TAKA LAKINI KWA SASA LIMEGEUKA NEEMA KWA WAKAZI HAO KWANI SAMBAMBA NA UWEPO WA MITI HUPANDA MAHARAGE NA MAHINDI KISHA KUGAWANA KWA AJILI YA CHAKULA.
Akiwasilisha Taarifa ya Mradi wa Shamba la miti unaotekelezwa na walengwa wa mpango wa TASAF Mtaa wa Mwinyi wilayani Kasulu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Vumilia Simbeye amesema katika kipindi cha mwaka wa Fedha 2022/2023 jumla ya miradi 106 ilitambuliwa ikiwa imegawanyika katika sekta za Mazingira pamoja na ujenzi wa Miundombinu.
Ameendelea kusema mpango huo umeendelea kuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wengi wanaotoka katika kaya masikini na kuwafanya kumudu gharama ndogondogo za maisha sambamba na kusomesha watoto.
Abdallah Ibrahim mkazi wa Kasulu mji, ambaye pia ni mnufaika wa mpango huo amesema kupitia fedha wanazopata wao kama wanufaika katika kata ya Mwinyi, wameanzisha kilimo cha miti na mazao ya chakula katika eneo lililokuwa likitumika kihifadhia taka mjini hapo.
Leticia Kagabo ambaye pia ni mnufaika wa TASAF amesema fedha aliyoipata kupitia mpango huo imemuwezesha kusomesha watoto wawili pamoja na kupata fedha ya pango, huku akisisitiza wanufaika wengine kutotumia fedha hizo kwa kufanya starehe au mambo mengine yaliyo nje ya malengo ya serikali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa