#
Baadhi ya Boti za kisasa zilizokabidhiwa kwa wavuvi mkoani Kigoma na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.
Wananchi wanaojishughulisha na Uvuvi katika Ziwa Tanganyika wameonesha kuridhishwa na hatua ya Seikali kusitisha kwa muda wa miezi mitatu shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika ili kulipa nafasi ya kuongeza kiwango chake cha uzalishaji wa Samaki.
Hatua hiyo muhimu imefikiwa wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vizimba vya kufugia Samaki, boti za kisasa za uvuvi na za doria pamoja na zoezi la utoaji wa Elimu kwa wavuvi kuhusu umuhimu wa upumzishaji wa shughuli za uvuvi kwa muda katika ziwa Tanganyika, iliyofanyika katika Mwalo wa Katonga katika manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani hapa.
Akikabidhi vitendea kazi hivyo kwa walengwa wanaofanya Shughuli za Uvuvi katika ziwa hilo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu ametoa zana hizo ili kuwezesha wananchi kufanya ufugaji wa kisasa ikiwa ni njia mbadala ya kujipatia kipato katika kipindi ambacho ziwa hilo litakuwa limepumzishwa.
Aidha Waziri Ulega amewataka wanufaika wa vitendea kazi hivyo kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa huku akiwataka maafisa uvuvi katika ukanda wa ziwa Tanganyika kuongeza kasi ya utoaji wa Elimu kwa wavuvi na wakazi ili waweze kushiriki katika kufanukisha zoezi hilo.
Mara baada ya kushuhudia ugawaji huo wa vitendea kazi, Mbunge wa Kigoma Mjini Mhe. Kirumbe Ng’enda amesema upumzishwaji wa Ziwa hilo umezingatia muda ambao ziwa hupunguza uzalishaji wake.
Amesema kuwa, kwa muda mrefu wavuvi wamekuwa wakitumia gharama kubwa kubwa bila kupata faida kutokana na kiwango cha upatikanaji wa samaki katika ziwa hilo kup[ungua na kusababisha kupata hasara.
Upande wake mbunge wa Kigoma Kusini Nashon Bidyanguze amesema ukosefu wa Elimu ya umuhimu wa upumzishaji wa ziwa hilo ulichangia kwa kiasi kikubwa kususa sua kwa zoezi hilo katika kipindi cha nyuma, lakini kwa sasa wavuvi na wakazi kwa ujumla wanaelimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kufungwa kwa ziwa Tanganyika.
Katika hafla hiyo, Waziri Ulega amekabidhi vizimba 29 kwa vikundi sita na watu binafsi 16 sambamba na boti kwa ajili ya uvuvi na doria katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.
Hafla hiyo imehuduriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, wabunge wa Majimbo ya Kigoma Mjini na Kigoma Kusini, Kamati ya Usalama Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, watendaji wa Serikali sambamba na wadau mbalimbali wa shughuli za uvuvi mkoani hapa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa