Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye amewaasa wanaume mkoani hapa kujitokeza kwa wingi na kuwa mstari wa mbele katika kuziendea huduma za upimaji wa Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili kujua hali zao kiafya kwa lengo la kupunguza maambukizi na athari kwa waliokwisha ambukizwa ugonjwa huo.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo, alipozungumza na wananchi wa mkoa wa Kigoma waliojitokeza kushiriki maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Kakonko.
Amesema wanaume wengi wameendelea kuishi kwa hofu huku wakiogopa kuujua ukweli kuhusu hali zao kiafya jambo ambalo ni hatari kwa waliokwisha pata maambukizi kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kwa sababu ya kuchelewa kuanza kutumia dawa za kufubaza makali ya maradhi hayo.
‘‘Nyote mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kwa kuongozana na wenzi wenu wa ndoa kupima hali zenu kiafya na iwapo nyote au mmoja wenu atabainika kuwa na maambukizi aanze kupata matibabu mapema na kujihakikishia Afya njema na maisha yenye furaha’’ amesema Andengenye.
Ameongeza kuwa, kati ya wanaoishi na VVU wenye Umri wa Miaka 15 hadi 64, wanaoendelea kutumia dawa na Asilimia 98.5 wanaonyesha kufanikiwa kufubaza maradhi hayo ambapo wanawake ni Asilimia 98.5 na Wanaume ni Asilimia 98.5.
Aidha, Mkuu wa Mkoa Amesisitiza kuzingatia Kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka 2022, kwani ujumbe wake unalenga kuimarisha hali ya usawa na kuondoa vikwazo katika Nyanja zote zinazotekeleza Afua mbalimbali za kupambana na kudhibiti Maambukizi ya VVU na Ukimwi pamoja na Jamii.
Awali akitoa taarifa ya Mkoa kuhusu maendeleo ya Utekelezaji wa Afua mbalimbali za UKIMWI, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Jesca Lebba, amesema Serikali inaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu mbalimbali ya Afya hasa katika upimaji wa Virusi vya Ukimwi.
‘’Hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa katika kuhamasisha na kuhakikisha wananchi wanatambua umuhimu wa kujua Afya zao na wenye maambukizi wanakuwa na utayari wa kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi, jambo ambalo tunaendelea kulitekeleza kwa mafanikio makubwa’’amesema Dkt. Lebba.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushiriki Maadhimisho hayo, wamekiri kuwepo kwa tatizo la muitikio hasi kwa wanaume wengi katika kuziendea huduma za upimaji wa virusi vya Ukimwi hususani katika Maeneo ya vijijini.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa