WANANCHI WA MKOA KIGOMA WAMEJITOKEZA KATIKA KUPATA MATIBABU KUTOKA KWA MADAKTARI BINGWA
Posted on: May 22nd, 2017
Mamia ya wananchi wa Mkoa Kigoma wamejitokeza katika kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa , mpango unaoratibiwa na Mfuko wa Taifa wa bima ya afya nchini (NHIF).
Matibabu hayo yanayotolewa katika hopsitali ya Mkoa Kigoma Maweni yanahusisha magonjwa ya kina mama ,magonjwa ya moyo,magonjwa ya watoto ambayo madaktari bingwa wake watafanya kazi hiyo moja kwa moja huku magonjwa mengine ambayo hayana madaktari bingwa yatatolewa ushauri wa hatua za kuchukua.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya mfuko huo, Anne Semamba Makinda amesema kuwa hakuna mtanzania atakayekufa kwa sababu ya kukosa pesa za matibabu kutokana na serikali ya awamu ya tano kuweka mfumo mzuri unaohakikisha wananchi wote wanapata matibabu kwa gharama nafuu.
Mama Anne alisema kuwa kwa sasa wananchi wote wataweza kujiunga na huduma za matibabu za mfuko huo kupitia makundi mbalimbali yalipo kwenye jamii na mitaa na wananchi watapata huduma za matibabu nchi nzima bila kubagua hospitali.
Aliongeza kuwa pamoja na hilo mfuko huo unatambua kuwepo kwa changamoto za uhaba wa madawa, vitendea kazi, uchache wa majengo na vifaa vingine vya kutolea tiba na kwamba mfuko huo umzingatia changamoto hiyo na kwa sasa mfuko unatoa mikopo kwa vituo vya afya, zahanati na hospitali ili kuwezesha huduma bora kupatikana wakati wote.
Akizungumzia utoaji huduma kwa wagonjwa alisema kuwa mfuko unapokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na lugha mbaya na za kuudhi zinazotolewa na watoa huduma na kwamba ikithibitika kwamba yupo mtoa huduma ametoa lugha mbaya kwa wagonjwa watachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernad Konga alisema kuwa mfuko unatambua changamoto iliyopo ya uhaba wa madaktari bingwa uliopo nchini na ndiyo maana mfuko umeanzisha mpango wa huduma za madaktari bingwa wanaotembea ili kuweza kuwafikia wananchi.
Pamoja na kutoa huduma kwa wananchi Bw. Konga alisema kuwa mpango huo pia unalenga kutoa mafunzo kwa watoa huduma waliopo kwenye vituo ambavyo mpango huo unatekelezwa ili waweze kuendeleza huduma husika baada ya madaktari bingwa hao kuondoka.
Alisema kuwa tangu kuanza kwa mpango huo jumla ya wananchi 13,000 wamefikiwa na kati yao zaidi ya 600 wamepatiwa huduma za upasuaji wa magonjwa mbalimbali na hivyo kufanikisha mpango wa kuwafikia wananchi kwa karibu.
Akisoma hotuba kabla ya kuzindua mpango huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Bw. Samson Anga alisema kuwa kumekuwa na uhitaji wa madaktari bingwa Mkoani humo ikizingatiwa kuwa kwa sasa mkoa unao madaktari bingwa wawili tu jambo ambalo linafanya wananchi kutumia muda na gharama kubwa kutafuta huduma hizo nje ya mkoa.
Katika hotuba hiyo Mkuu wa wilaya Kigoma,Samosn Anga alisema kuwa mpango huo ni wa maana sana kwani utawasaidia wananchi wa mkoa huo kupunguza makali ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wakati huu na kwamba serikali ya mkoa itatoa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha utekelezaji wa mpango huo unakuwa wa mafanikio.