Takribani Walimu 635 wamepatiwa mafunzo ya uwezeshaji wa Walimu elimu ya awali katika Mkoa wa Kigoma. Mafunzo hayo kabilishi yanahusu Mtaala wa Elimu ya awali ulioboreshwa mwaka 2016 ambao utaanza kutumika rasmi mwaka 2017. Mtaala huu unasisitiza ujenzi wa umahiri kwa mtoto na unawezesha kutawala na kupambana na changamoto katika mazingira yake. Kupitia Mtaala huu Walimu wataweza kujenga umahiri katika kutekeleza Mtaala husika ili kufikia lengo la Serikali la kutoa Elimu bora kuanzia ngazi ya Elimu ya awali hadi Elimu ya Juu. Kuimarika kwa ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya awali kutajengea watoto utayari wa kujifunza na hivyo kurahisisha uelewa wao katika ngazi zingine za Elimu. Akizungumza katika hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga amesema mafunzo hayo muhimu kwa Walimu wanaofundisa elimu ya awali yatawajengea uelewa mzuri wa Mtaala wa Elimu ya awali kabla ya kwenda kutekeleza mtaala huo, kuwawezesha kuchambua mtaala wa Elimu ya Awali na kupata mbinu za kufundishia elimu ya awali ili kuweza kuwa na mbinu bora na uwezo wa kuimarisha ujenzi wa umahiri katika maeneo ya ujifunzaji yanayojikita katika Kuhusiana, Kuwasiliana, Kumudu stadi za kisanii, kutumia dhana za kihisabati, kutunza afya na kutunza mazingira wakati wa mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji. Brigedia Jeneral Maganga ameishukuru na kuipongeza Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) pamoja na Mpango wa LANES kwa kuchukua hatua hii muhimu ya kuandaa mafunzo kabilishi kwa walimu wanaofundisha watoto wa Elimu ya Awali. Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kutoa elimu bora katika kila ngazi ya elimu kwa kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia shuleni, elimu inayonuia kuwaandaa vijana watakao endana na nchi ya viwanda, wasomi watakaojenga na kuendeleza Uchumi wa Taifa.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa