Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 ngazi ya Mkoa wametakiwa kutanguliza uzalendo, weledi na uadilifu katika kazi wanayoifanya ili iweze kulisaidia Taifa kufikia malengo yaliyowekwa huku wakiacha alama iliyotukuka katika utendaji kazi.
Akikagua mafunzo ya mazoezi kwa vitendo yanayofanywa na Wakufunzi wa Sensa hiyo katika Kata ya Kidahwe Wilaya ya Kigoma Vijijini, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye amewasisitiza kuifanya kazi hiyo kwa ukamilifu ili kuepuka kujitokeza kwa dosari zozote.
Amesema ameridhishwa na Mafunzo yaliyotolewa kutokana na Wanamafunzo kuonesha uwezo mkubwa kwenye mazoezi ya vitendo, huku akiwaasa kuhakikisha zoezi litakapoanza taarifa zitakazohitajika zijazwe kwa usahihi na ukamilifu.
Aidha, amewasihi kuheshimu Mila na Desturi za wakazi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo ili kudumisha mahusiano mema baina yao na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa zoezi hilo hali itakayoruhusu upatikanaji wa taarifa zinazohitajika kwa urahisi na usahihi.
Mafunzo hayo yamelenga kupima uelewa wa wakufunzi hao kutokana na mafunzo ya nadharia waliyoyapata pamoja na kupima ufanisi wa viendea kazi ili kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza kabla ya kuanza kwa mafunzo ya Makarani wa Sensa na zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa