WAKIMBIZI KUTOKA BURUNDI MKOANI KIGOMA WAANZA KUREJEA KWAO
Posted on: September 7th, 2017
Kundi la kwanza la wakimbizi 301 wa Burundi waliokuwa wakihifadhiwa Nchini Tanzania kwenye kambi ya Nduta wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma limeanza kurejea nchini Burundi huku viongozi wa nchi hizo mbili wakisema kuwa ni heshima kubwa kwa wakimbizi hao kurudi nchini kwao sasa.
Mkuu Wa Mkoa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliongoza uzinduzi rasmi wa zoezi hili huku akisema kuwa takribani wakimbizi 12,000 wanatarajia kurudishwa kwao hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Alisema kuwa kwa sasa wakimbizi hao watarejeshwa kwa hiari kulingana na mikataba ya kimataifa ya kuhifadhi na kurejeshea kwao wakimbizi ambayo Tanzania imeridhia.
Awali Mratibu wa Idara ya Wakimbizi kanda ya Magharibi Nchini Tanzania, Bw. Tonny Laizer alisema kuwa kwa sasa wakimbizi watakaorejeshwa ni wale watakaojitokeza na kuandikishwa kwa hiari kurudi kwao.
Laizer aliongeza kuwa awamu ya pili ya zoezi hilo litafanyika kwa uhamasishaji kwa viongozi Wa serikali ya Burundi kutembelea makambi kuzungumza na wakimbizi hao sambamba na baadhi ya wakimbizi kupelekwa kutembelea Burundi kuona hali ya amani na usalama iliyopo nchini humo ili kuwashawishi wakimbizi wenzao kujiandikisha kurudi nchini mwao kwa hiari.
Kwa upande wake Makamu Waziri wa mambo ya ndani wa Burundi, Terence Ntahiraja akinukuu maneno aliyotoa Raisi Pierre Nkurunzinza wa Burundi Julai 19 mwaka huu Ngara Mkoani Kagera nchini Tanzania kuwa Burundi ina amani ya uhakika na watu hao hawana sababu ya kuishi uhamishoni kama wakimbizi.
Ntahiraja alisema kuwa baadhi ya wakimbisi ambao hawako tayari kurudi kwa madai ya hali ya amani haijatengemaa nchini humo wanayo fursa kwenda kutembea kuona hali halisi na kuamua huku akionya baadhi ya wakimbizi wanaohamasisha wakimbizi wenzao wasirejee kwa kigezo cha hali mbaya ya usalama.
Kuhusiana na hali ya kiuchumi ya wakimbizi hao Waziri huyo wa mambo ya ndani alisema kuwa serikali ya Burundi inaweka mazingira mazuri kwa wakimbizi hao kurejea kwenye maisha yao kawaida kwa kuandaa mipango ambayo itakuwa na msaada wa kiuchumi kwa wakimbizi hao.
Dafroza Mugabekazi na Mwamvita Emanuel ni miongoni mwa wakimbizi walioanza safari ya kurudi Burundi ambapo wamesema kuwa wameamua kurudi Burundi kujenga maisha yao baada ya amani kurudi huku wakieleza kuchoshwa na maisha ya ukimbizi.