Wakazi Mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya maambukizi ya Magonjwa mbalimbali ya mlipuko yanayoripotiwa kujitokeza ndani ya Mkoa pamoja na Nchi jirani.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ametoa kauli hiyo leo Tarehe 25 Oktoba 2022 wakati akifungua kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi Mkoa na kusisitiza kuwa, wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi ya Surua na Kipindupindu yaliyoripotiwa kuwepo mkoani hapa pamoja na ugonjwa wa Ebola uliopo nchi jirani ya Uganda.
‘‘Mkoa wa Kigoma unamuingiliano mkubwa na wageni kutoka nchi za jirani ikiwemo Nchi ya Uganda kupitia mkoa wa Kagera, hivyo wananchi mnatakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola na iwapo mtabaini dalili zozote za ugonjwa huo taarifa zitolewe mapema ili kupunguza madhara makubwa yanayoweza kujitokeza katika jamii’’ alisema Andengenye.
Aidha Mkuu wa Mkoa amezungumzia maendeleo ya utoaji chanjo ya UVIKO 19 kimkoa na kufafanua kuwa, Mkoa umefanya vizuri katika Sula la utoaji wa Chanjo hiyo huku matarajio yakiwa ni kuwafikia walengwa wote 1,375,735 ikiwa ni sawa na Asilimia 100 ya Wananchi wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, ifikapo Tarehe 31 Desemba 2022.
‘‘Mpaka sasa tumefanikiwa kutoa chanjo jumla ya walengwa 1,265,274, sawa na Asilimia 92, huku lengo la kampeni likiwa ni kuchanja walengwa 110,458 ili tuweze kufikia Asilimia 100 ya walengwa wote’’ alisema Andengenye.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa Rai kwa viongozi wa Serikali, dini, Kamati za Ulinzi na Usalama, wanahabari, wasanii na wawakilishi mbalimbali wa makundi ya kijamii kuendelea kuhamasisha wananchi katika maeneo yao ili waweze kujitokeza na kupata chanjo kwa lengo la kujikinga dhidi ya UVIKO 19.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua kikao hicho, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba, amesema Idara ya Afya imeendele kutekeleza Kampeni mbalimbali za kupambana na kudhibiti Maradhi ya Mlipuko ikiwemo kipindumbindu, Surua pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
‘‘Mpaka sasa tumefanikiwa kuchanja Asilimia 95 ya walengwa wa chanjo ya UVIKO, huku tukiendelea kuchukua tahadahri dhidi ya ugonjwa wa Surua. Aidha kwa upande wa Ebola, Mkoa hauna changamoto hiyo japo tumejiandaa kwa kuchukua tahadhari na kutenga maeneo ya kukabiliana na ugonjwa huo iwapo utabainika kujitokeza’’ Alisema Dkt . Lebba.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa