Wakazi Mkoani Kigoma wametakiwa kuendeleza shughuli za ujenzi huku wakichukua tahadhari dhidi ya uharibifu wa Mazingira na kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa maisha ya sasa na kwa vizazi vijavyo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo alipofika mkoani hapa kwa lengo la kutoa maelekezo kuhusu zuio la Serikali la kutokuendeleza makazi katika Kata ya Sanganigwa iliyopo manispaa ya Mji Kigoma-Ujiji ambapo aliidhinisha kuendelea kwa shughuli hizo kufuatia Serikali kujiridhisha kuhusu kutowepo kwa athari za kimazingira katika eneo hilo.
Alisema maeneo yote ambayo wananchi wanataka kuendeleza makazi na shughuli nyingine za maendeleo zinazohusisha ujenzi, wahakikishe wanapata ushauri kutoka kwa wataalam wa ujenzi na wale wa mazingira ili kuepusha athari zitokananzo na shughuli hizo.
‘‘Baadhi ya Wataalam ama kwa uzembe au kutokujua wamekuwa wakiruhusu wananchi kujenga katika vyanzo vya Maji, maeneo ya uhifadhi na hata maeneo hatarishi kwa usalama, bila kutoa maelekezo yanayoambatana na ushauri pamoja na tahadhari.’’ Alisema Jafo.
Aliwaagiza wataalam wa Mazingira kutoa ushauri na maelekezo kwa Serikali na pamoja na wananchi pale wanapoona kunampango wa uanzishwaji wa shughuli za kibinaadam katika eneo ambalo uharibifu wa kimazingira unaweza kutokea ili kuepusha usumbufu na hasara zinazoweza kuwakuta wananchi wa eneo hilo.
Aidha Waziri Jafo alielekeza Ujenzi unaofanyika maeneo yote nchini uzingatie utaratibu wa uvunaji wa Maji ya Mvua kwa lengo la matumizi ili kupunguza gharama na matumizi makubwa ya maji katika makazi.
‘’Naelekeza maeneo yote ya Majiji, Miji, Manispaa na wilaya ujenzi wa makazi uambatane na utaratibu maalum wa uvunaji Maji ya mvua kuliko kuyaacha yapotee bure huku tunauhitaji mkubwa wa Maji hayo kwa matumizi yetu’’alisema Waziri Jafo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa