Serikali kupitia imelipa fidia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.68 kwa wakazi wanaoishi eneo lililokuwa Kitongoji cha Kabukuyungu na Mahasa katika Kijiji cha Kalilani Kata ya Buhingu Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma kutokana na eneo hilo kuwa chini ya umiliki wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale.
Zoezi hilo limefanyika ili kupisha uhifadhi wa Mazingira endelevu kwa ajili ya hifadhi ya wanyama jamii ya Sokwe ambapo kwa hatua ya awali jumla ya kaya 205 kati ya kaya 376 ambazo wakazi husika waliridhia kufanyiwa Tathmini ya mali zao zimelipwa huku uongozi wa Serikali ya Mkoa ukitoa Rai kwa kaya ambazo hazijafanyiwa tathimini kuchukua hatua ili kuepusha hasara ikiwemo kupoteza makazi yao baada ya Siku Sitini kuanzia Februari 25,2025 ambapo maeneo hayo yatarejeshwa rasmi kwenye umiliki wa Hifadhi hiyo.
Zoezi la ulipaji wa fidia, limeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, ambapo ameitaka jamii kuendelea kulinda Mazingira na viumbehai ikiwemo wanyamapori katika maeneo ya hifadhi ili kudumisha urithi huo wa Asili kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Amesema wakazi wanapaswa kutambua umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi ikiwemo mnyama Sokwe, ambao wanazidi kuadimika nchini kutokana uharibifu wa Mazingira huku akisisitiza ulinzi wa hifadhi ya Mahale na maeneo mengine tengefu mkoani Kigoma kwa ajili ya kutunza Mazingira na kudumisha Sekta ya Utalii ambayo inamchango mkubwa katika pato la Taifa.
Afisa Mhifadhi Mkuu Kharidi Mgofi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Mahale, amepongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kuwabadilishia eneo la makazi wananchi hao kulikoenda sambamba na malipo ya fidia kwa kuwa kimsingi eneo hilo lilikuwa chini ya umiliki wa hifadhi tangu awali kabla ya kugeuzwa makazi.
Aidha baadhi ya Wananchi, walionufaika na Mpango huo, wameupongeza uongozi Mkoa chini ya Utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita kutekeleza zoezi hilo kwa kuzingatia utu, jambo litakalowafanya kutohangaika watakapohamia katika makazi mapya.
Aidha, wakazi hao wamesema, hatua hiyo imeondoa sintofahamu iliyokuwa ikiwakabili na kusababisha kusimama kwa shughuli za Maendeleo ambapo mara baada ya malipo hayo wameahidi kutekeleza agizo hilo kwa kuhamia maeneo waliyotengewa ili kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa