Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewataka wajumbe wa mabaraza ya Ardhi na Nyumba mkoa wa Kigoma kuzingatia kanuni na maadili na miongozo ya utendaji kazi ili kutoa haki kwa wananchi wenye changamoto za migogoro ya ardhi mkoani Kigoma.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo mara baada ya kuwaapisha wajumbe wa mabaraza hayo kwa wilaya za Kakonko, Uvinza na Buhigwe na kuwataka kuepuka rushwa, upendeleo au kushiriki vitendo vyovyote vitakavyoashiria uvunjani wa sharia katika utoaji maamuzi dhidhi ya walengwa.
‘’Wajumbe niwasisitize kiapo mlichoapa mkakitendee haki kwa kuepuka kutoa maamuzi na maoni kwa kuzingatia hisisa na mihemko bali kwa kuzingatia miongozo na ushahidi toshelevu unaotolewa ndani ya mabaraza’’
Amewasisitiza wajumbe hao kujenga tabia ya kusoma na kuelewa Sheria ndogo za mabaraza ili ziweze kuwa miongozo katika kufanya maamuzi hali itakayowaepusha na lawama zitakazotokana na kulalamikiwa kwa kufanya upendeleo.
Aidha kupitia kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amemuelekeza Katibu Tawala Mkoa kuhakikisha wajumbe wa mabaraza hayo katika Halmashauri za Uvinza na Kakonko wanapatiwa Ofisi katika maeneo ya makao makuu ya Halmashauri na uwepo wa ofisi hizo utangazwe ili kuwarahisishia wananchi kutambua maeneo ya upatikanaji wa huduma hizo.
Nisisikie kuwa kuna wajumbe wa baraza la Ardhi na Nyumba wamekosa ofisi na hakikisha uwepo wa ofisi hizo unafahamika kwa wananchi ili wasiendelee kusumbuka kufuata huduma mbali na maeneo yao ya makazi.
Upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria Mkoa Diana Chove, amewataka wajumbe wa mabaraza hayo kujenga tabia ya kutafakari kwa kina kabla ya kutoa maamuzi kuhusiana na mashauri wanayoyaamua ili kuharakisha upatikanaji wa suluhu.
Aidha amewakumbusha wajumbe hao kutoingilia majukumu yasoyowahusu bali wasimamie yale yaliyomo kwenye miongozo ya utendaji kazi wao.
Jumla ya wajumbe saba wa mabaraza hayo wameapa mbele ya mkuu wa mkoa wa Kigoma leo Mei 17,2024 kupitia hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kuendana na Sheria ya Mahakama ya Ardhi Na. 2 ya Mwaka 2002 chini ya Kanuni Namba 36(1) na (2) GN na 174/2003.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa