Wananchi mkoani hapa wamehimizwa kuendelea kushirikiana katika kuimarisha Umoja na Mshikamano huku wakiwaenzi waasisi wa Taifa kwa kudumisha Amani iliyopo nchini ambayo ni chachu ya Maendeleo tuliyonayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali Michael Masala kupitia Hotuba aliyoitoa alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka sitini na Moja ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Amesema Msingi wa Amani, Umoja na Mshikamano tulionao ambao uliwekwa na waasisi wa Taifa letu ni chachu kubwa ya maendeleo tuliyoyafikia kama Taifa hivyo hatuna budi kuuendeleza na kuudumisha.
‘‘Tusikubali kuichezea Amani tuliyonayo na tunapaswa kuilinda kwa gharama yoyote ili tusije kuupoteza Uhuru tulionao sasa, kwani bila kuwa huru hakuna uwepo wa maendeleo ya kweli’’Amesema Masala.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Gabriel, amesema nchi nyingi zinaonekana ziko Huru lakini hazina Amani ya kweli, hali inayosababisha kukosekana kwa utulivu wa wanchi katika kutekeleza majukumu yao ya kimaendeleao.
‘‘Tanzania imekuwa ni nchi Huru na yenye Amani ya kweli tangu ilipopajipatia Uhuru wake miaka 61 iliyopita na wananchi wanaendelea kutekeleza majukumu yao na kuishi kwa furaha, hivyo tuendelee kuitunza amani hiyo kwa mustakabali wa Maendeleo ya Taifa letu’’ amesisitiza Gabriel.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza na kushiriki katika Maadhimisho hayo, wamepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na viongozi wa Ngazi mbalimbali Serikali wakiongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu, kwa kuhakikisha amani iliyopo inadumu na kutoa fursa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo huku wananchi wakiendelea kuishi kwa furaha na upendo.
Aidha wakazi hao wamesisitiza kuendelea kuyaenzi mawazo makuu ya Muasisi wa Taifa Mwal. Julias Kambarage Nyerere kwa kupambaana na maadui Ujinga, Maradhi na Umasikini kwa kuhakikisha wanashiriki kwa dhati katika shughuli zote za maendeleo zinazotekelezwa kupitia miradi mbalimbali ya Serikali.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria na kushiriki maadhimisho hayo wakiwemo wakuu Taasisi za Kiserikali, Binafsi na zile za kidini pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kigoma ambapo kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa Mwaka 2022 ikiwa ni ‘’AMANI NA UMOJA NI NGUZO YA MAENDELEO YETU’’
PICHA: BAADHO YA WAKUU WA TAASISI ZA SERIKALI, TAASISI BINAFSI, VIONGOZI WA DINI, SIASA PAMOJA NA WANANCHI WALIOJITOKEZA KUSHIRIKI KATIKA KILELE CHA MADHIMISHO YA UHURU WA TANZANIA BARA YALIYOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO KATIKA HALMASHAURI YA MJI WA KASULU LEO TAREHE 9 DESEMBA 2022.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa