Wadau wa Viwanda Mkoa wa Kigoma wametakiwa kutumia Falsafa ya KAIZEN ili kuboresha hali ya utendaji kazi na kuimarisha uwezo katika uzalishaji wa bidhaa zitakazomudu ushindani katika Soko la Ndani na Nje ya Nchi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Kigoma Sangu Deogratius, ametoa Rai hiyo alipokufungua Mafunzo yaliyoenda sambamba na uhamasishaji wa kutumia Falsafa ya KAIZEN katika Mkoa wa Kigoma, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Katibu Tawala Mkooani hapa.
Amesema ujenzi na Uchumi shindani unategemea ukuaji wa Sekta Imara ya viwanda na uwepo wa watendaji wenye ujuzi wakiwa na mtazamo unaozingatia uendelevu wa viwango bora na vyenye tija sambamba na uwezo wa kuihudumia Sekta hiyo.
‘‘Falsafa ya KAIZEN ndio Siri ya mafanikio ya nchi ya Japan katika uendeshaji wa viwanda na kujenga msingi imara wa kiuchumi unaolifanya Taifa hilo kuweza kuhimili ushindani wa Ubora wa Biashara katika Soko la Dunia’’ amesema.
Ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania imepokea kwa mikono miwili ushirikiano na Serikali ya Japan kupitia JICA katika utoaji wa Mafunzo ya Falsafa hiyo ili kujenga hazina ya Rasilimali watu kwa ajili ya kujenga uchumi imara na shindani kimasoko kwa Maendeleo ya Taifa.
Aidha amewasisitiza wadau kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika kutoa ushauri kwa wadau wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki kwa kueneza utamaduni mpya wa kufanya kazi viwandani kwa kufuata misingi ya falsafa ya KAIZEN.
Naye Deus John kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara ambaye pia ni Mkufunzi wa Falsafa ya KAIZEN, amesema Elimu hiyo imejikita katika kuwajengea uwezo wamiliki na wafanyakazi katika viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ili kufanya uzalishaji wenye ubora utakaoendana na mahitaji halisi ya soko la ndani nan je.
Amesisitiza kuwa, Elimu ya KAIZEN inalenga kuvumbua mawazo na maarifa yatakayosaidia kuboresha uzalishaji katika aina zote za viwanda, kuzalisha bidhaa zenye kiwango kinachokubalika katika Soko la Nje ili kuifanya nchi ya Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2030.
‘‘Katika mikoa ambayo elimu hii imetolewa tayari wadau wameanza kupata matokeeo chanya kwa kuepuka hasara katika uzalishaji, kuzalisha bidhaa bora zenye kuhimili ushindani wa soko la ndani na lile la kimataifa’’ amesema.
‘‘Tunaendelea kutoa elimu hii katika Taasisi za Serikali pia ili wateja waweze kunufaika na utolewaji wa huduma bora katika ofisi za Serikali kwa kuwajengea uwezo watoa huduma ili watambue namna bora ya kutoa huduma kwa wateja wao’’ Amesema Deus.
Pia Emanuel Mgunda, Mthibiti Ubora wa uzalishaji katika Kiwanda cha Tanganyika Pure Drinking Water kilichopo mkoani hapa, amesema mafunzo waliyoyapata yataongeza thamani na tija katika uzalishaji viwandani katika Mkoa wa Kigoma na kuongeza thamani ya bidhaa hali iitakayosababisha kupanua wigo wa masoko.
‘‘Mkoa wetu umepakana na nchi jirani za Congo na Burundi, hivyo kutokana na uwezo tuliojengewa tumepata maarifa yatakayotusaidia kukabiliana na ushindani uliopo ili tuweze kumudu kuuza bidhaa zetu katika nchi hizo’’ amesema Emmanuel.
KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana badilika kwa ubora au uzuri linalotumika kwenye biashara ambapo mpango huo unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Serikali ya Japan inayotoa misaada ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea JICA, kwa lengo la kuimarisha Viwanda vya Uzalishaji kupitia uboreshaji wa Tija na Ubora.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa