Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mhe. Thobias Andengenye akizungumza na waumini wa dhehebu la Anglican katika Kanisa la Mt. Andrea lililopo Kasulu Mjini aliposhiriki Ibada na kufungua Semina Maalum ya Ujasiriamali kwa wachungaji wa Dayosisi ya Western Tanganyika siku ya Tarehe 7 Mei, 2023.
Viongozi wa Madhehebu ya Dini mkoani Kigoma wamehimizwa kudumisha mafunzo na malezi bora ya kiimani kwa waumini wao ili kujenga Taifa lenye kizazi kitakachoenenda katika maadili mema na kujengeka katika misingi ya hofu na kumheshimu Mwenyezi Mungu.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobia Andengenye ametoa nasaha hizo aliposhiriki Ibada ya kusimikwa kwa Mchungaji Kanoni, Careb Zephania kuwa Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Wester Tanganyika Emmanuel Bwata pamoja na kufungua Semina Maalum kwa wachungaji wa Dayosisi hiyo.
Amesema ongezeko la vitendo vya ukatili katika Jamii, uwepo wa chuki na visasi baina ya ndugu, rushwa, dhuluma pamoja kuibuka kwa vitendo vya usagaji na ushoga ni ishara ya ukosefu wa hofu ya Mwenyezi Mungu.
Ameendelea kufafanua kuwa, viongozi wa dini wanapaswa kutokukata tamaa na kuongeza juhudi katika kulibeba jukumu la kuuelimisha na kuuadilisha Umma ili uweze kuyatambua makusudi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu na kuifanya Dunia kuwa Sehemu salama ya kuishi kwa kila Mtu.
Amesisitiza kuwa, Msingi wa Madhila ya kitabia na mienendo isiyo katika mfumo wa Tamaduni zetu tunayoishuhudia sasa isipokemewa na kudhibitiwa itaathiri kwa kiasi kikubwa kizazi chetu kijacho na kukifanya kuishi maisha yasiyo na utu, yaliyoja kufuru na machukizo mbele ya Mwenyezi Mungu na wanadamu wenyewe.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amepokea ombi la Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Emmanuel Bwata, kusaidiwa kupata mbegu na miche ya chikichi kwa ajili ya kutimiza azma ya Kanisa kuanzisha mradi mkubwa wa Kilimo cha zao hilo.
Amefafanua kuwa, Serikali mkoani Kigoma inatambua umuhimu mkubwa wa kuinua uchumi wa wananchi kupitia zao hilo hivyo hatua madhubuti zitachukuliwa ili kuhakikisha uzalishaji wa miche na mbegu za chikichi unafanyika karibu na mazingira ya wahitaji ili kuwapunguzia adha.
Pia Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Taasisi za kidini, vikundi mbalimbali vya waumini pamoja na watu binafsi kuanzisha vitalu vya zao la chikichi katika maeneo ya jirani na makazi yao na kuiarifu Serikali kupitia wataalam wa Kilimo ili waweze kupelekewa mbegu na kusaidiwa katika usimamizi wa uzalishaji wa Miche.
Ibada hiyo imefanyika Sambamba na zoezi la uchangiaji wa fedha na vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa Kanisa la Mt. Andrea Dayosisi ya Tanganyika Magharibi lililopo Kasulu Mjini, ambapo Mkuu wa Mkoa amechangia Jumla ya Shilingi laki Tano na kuahidi kiasi kama hicho cha Fedha kwa ajili ya kuchangia vikundi vya Wanawake wajasiliamali vinavyotarajia kuanzishwa na Kanisa hilo.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa