Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewaonya waajiri katika Sekta za Umma na binafsi mkoani hapa kuachana tabia ya kuwanyanyasa watumishi na kufuata Sheria na miongozo ya kazi wanazosimamia ili kulinda haki na stahiki za watumishi walio chini yao.
Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza na wafanyakazi wa Mkoa wa Kigoma kwenye kwenye Hafla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) iliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Amesema ni vizuri Menejimenti za Taasisi zikajiwekea utaratibu wa kukutana na viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi na kuweka mipango ya pamoja badala ya kuviona vyama hivyo kuwa ni maadui na kuvifanya kuwa daraja muhimu baina ya waajiri na waajiriwa.
Vyama vya wafanyakazi visibebe jukumu la kusimamia maslahi ya watumishi pekee bali vijikite pia katika kutoa Elimu, kusimamia kanuni na Sheria kwa watumishi sambamba na kujenga utaratibu wa kukutana mara kwa mara na pande zote mbili yaani waajiri na waajiriwa ili kutatua changamoto zinazojitokeza.
‘’mitazamo ya kujikita upande mmoja imekuwa ikichangia sana kukuza migogoro baina ya watumishi na waajiri wao hali inayosababisha uzoroteshaji wa matokeo chanya katika utendaji kazi na kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi’’ amesema.
Pia Andengenye amewataka watumishi kuendelea kupiga vita uvivu, rushwa, kuepuka vitendo vya utovu wa nidhamu, ubinafsi na kuongeza bidii na maarifa mapya katika utendaji kazi ili kuimarisha uchumi wao binafsi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewasisitiza watumishi wa Uma mkoani Kigoma kuendelea kuziamini taasisi rasmi za kifedha kwa kujiimarisha kiuchumi na kutimiza malemgo yao kupitia mikopo inayotolewa na Taasisi hizo huku akiwataka watendaji katika Taasisi hizo za kifedha kuendelea kupunguza riba za mikopo ili watumishi waweze kurejesha mikopo kwa muda muafaka.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha watendaji hao kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wananchi kugombea nyadhifa mbalimbali katika nafasi za uongozi.
kadhalika amewaasa watumishi kuendelea kufanya mapinduzi ya kifikra sambamba na kuongeza juhudi, nidhamu na maarifa katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi Katibu wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi mkoa wa Kigoma Jumanne Hamis ametoa wito kwa wafanyajkazi wote nchini kuongeza juhudi katika kufanya kazi zao huku wakizingatia weledi.
Kiongozi huyo ameiomba serikali kuwatazama upya baadhi ya wastaafu kutokana na kulipwa kiasi cha fedha kisichoweza kukidhi mahitaji yao ya kimaisha huku akitoa ombi la kwa serikali kuzielekeza Taasisi za kibenki kupunguza riba katika mikopo wanayotoa kwa watumishi pamoja na kuchukua hatua kali kwa baadhi ya waajiri katika Taasisi binafsi kutokana na kushindwa kuzingatia sheria ya ulipaji wa mishahara kwa ngazi ya kima cha chini kuendana na miongozo.
Kadhalika ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Samia Suluhu kwa kupandisha madaraja ya mishahara kwa watumishi wa Umma, kuondolewa kwa tozo ya Asilimia Sita kwenye mikopo ya Elimu ya Juu, kuongeza umri wa wategemezi kutoka miaka 18 hadi 21.
Aidha pongezi hizo zimehusisha serikali kushughulikia maslahi ya watumishi walioondolewa kazini kwa kugushi vyeti pamoja na kulipa madeni ya mishahara ya walimu.
Kupitia hotuba hiyo, Katibu huyo ameiomba serikali kurejesha kikokotoo cha Asilimia Hamsini kwa moja chini ya mia tano arobaini kwa mshahara wa mwisho badala ya kutumia mfumo wa kutafuta mshahara bora wa miaka mitatu ya utumishi huku akisisitiza kufuatilia utendaji kazi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kufuatilia michango ya watumishi kwa waajiri na kusababisha changamoto na mgogoro mkubwa baina ya mwajiri na mwajiriwa.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi kimkoa kwa mwaka 2024 yanakaulimbiu isemayo ‘’Nyongeza ya Mishahara ni msingi wa kuongeza ufanisi na Tija katika utoaji wa Huduma na uzalishaji mali kwa ajili ya Maendeleo ya Jamii’’
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa