Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye amevitaka vyama vya Wafanyakazi Mkoani hapa kuwa daraja muhimu la kutatua changamoto baina ya waajiri na waajiriwa badala ya kuwa sehemu ya kuwachunguza, kuwashtaki na kuwanyanyasa watumishi wanaowawakilisha.
Amesema vyama hivyo vinapaswa kuzingatia usawa katika kusimamia haki za waajiri na waajiriwa ili kudumisha utendaji kazi wenye msingi wa kuleta matokeo chanya kwa Umma na upatikanaji wa maslahi kwa Watendaji.
Kauli hiyo ameitoa alipozungumza na maelfu ya wafanyakazi kutoka Taasisi za Umma na zile za Binafsi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kimkoa katika wilaya ya Kakonko mkoani hapa.
Amesema waajiri na waajiriwa wanapaswa kuendelea kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri kwani mahali popote pa kazi penye mahusiano mema, ujira mzuri na ulio halali lazima panakuwa na mafanikio na ufanisi katika uzalishaji au utoaji wa huduma.
Amesema wafanyakazi hususani katika Sekta za Umma wanapaswa kuongeza juhudi kiutendaji kazi kwani ni mashuhuda wa namna ambavyo Rais wa Jamhuri ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyothamini utendaji kazi wao kwa kuendelea kubooresha maslahi yao ikiwa ni pamoja na kupandisha mishahara na madaraja katika ngazi mbalimbali za kiutumishi.
Kupitia hotuba yake, Andengenye amewataka wafanyakazi kujiimarisha katika matumizi ya Teknolojia pamoja na kujiwekea sera za kupambana na umasiki ili kutoa huduma bora na kuzalisha bidhaa zitakazomudu ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafanyakazi mkoani Kigoma kushiriki kikamilifu mchakato wa uchaguzi kwa kujiandijisha na kupiga kura sambamba na kuihamasisha jamii kushiriki zoezi hilo kwa hali ya amani na utulivu.
Katika hatua nyingine Andengenye amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma kufuatilia na kuwasimamia waajiri wote ili kuhakikisha wanawasilisha michango ya watumishi katika Mifuko ya hifadhi za jamii huku akiwataka waajiriwa kutumia Teknolojia kufuatilia hali ya uwasilishwaji na mapokezi ya michango hiyo.
Amesema kwa kufanya hivyo itawapunguzia usumbufu watumishi wanapotamatisha mikataba ya ajira katika mafao yao.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa