BAADHI YA MASHINE ZILIZOPO KATIKA KIWANDA KIDOGO CHA VIJANA, KIKUNDI KAZI-IPOSA KILICJOPO MJINI KASULU.
Vijana wilayani Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuchangamkia fursa ya Mikopo inayotolewa na Serikali kwa makundi ya vijana, wanawake na walemavu, kutokana Asilimia Kumi ya Fedha inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kauli hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Komredi Sahili Nyanzabala Geraruma, alipokagua na kuzindua Kiwanda kidogo cha vijana, Kikundi kazi-IPOSA kinachojishughulisha na kazi za useremala na uchomeleaji wa vyuma kilichopo katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Amesema vijana wengi mitaani wanaujuzi wa kufanya kazi mbalimbali halali za uzalishaji lakini changamoto kubwa wanashindwa kufuata taratibu zilizowekwa na serikali ili kupata mikopo hiyo.
‘‘Nawashauri vijana wenzangu, bainisheni shughuli mnazotaka kuzifanya kwa ajili ya kujitafutia riziki kisha fuateni taratibu zinazotakiwa ili muweze kupata mikopo hiyo na mkajiinue kiuchumi’’
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, ameupongeza uongozi wa Serikali ya Mji wa Kasulu kwa ubunifu na usimamizi walioutoa kwa vijana hao, huku akisisitiza Halmashauri Kuendelea kutenga maeneo kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ya vijana.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kasulu mjini ambaye pia ni Waziri wa Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, amesema vijana wajitahidi kukopa kwa malengo na wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wahitaji wengine wanaotaka kukopa.
‘‘Tuwe na malengo katika ukopaji wetu na tujitahidi kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na itakapotokea tumeshindwa kurejesha basi tutoe taarifa kwa uongozi ili watupe utaratibu mzuri wa kufanya badala ya kukimbia deni’’
Nao vijana wa hao wa kikundi kazi-IPOSA, hawakusita kuishukuru serikali kwa kuwapa mkopo wa Fedha kiasi cha Shilingi Milioni mia moja ishirni na tano, Ushauri, Ardhi na Miongozo ya namna bora ya kutekeleza majukumu yao katika uendeshaji wa Mradi huo.
‘‘Mradi huu umetuheshimisha katika familia zetu na jamii kwa ujumla na kututoa katika orodha ya wazururaji na watu wasio na kipato cha uhakika, kwani kwa sasa tunaendesha maisha yetu vizuri na kutekeleza mipango mingine ya maendeleo’’ amesema Batholomeo Joel.
Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru mkoani Kigoma zimehitimisha Siku ya Tano ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, zimezindua na kuweka jiwe la msingi jumla ya Miradi sita yenye Thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni Mia saba hamsini ikiwemo Mradi wa Maji Mganza, Barabara ya Lami Kumsenga, vyumba vitatu vya Madarasa katika shule ya Msingi Kumnyika, Nyumba ya watumishi wa Afya katika Zahanati ya Kijiji Mwibuye na Kikundi cha Vijana-IPOSA Kalema.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa