MKUU WA MKOA WA KIGOMA KAMISHNA JENERALI MSTAAFU WA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI THOBIAS ANDENGENYE AKIFUATILIA JAMBO WAKATI ALIPOKUTANA NA KUZUNGUMZA NA UJUMBE KUTOKA KWA MKANDARASI CHINA RAILWAY ENGINEERING GROUP CO. LTD.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amemtaka Mkandarasi anayetekeleza kazi ya upanuzi na ukarabati wa Kiwanja cha Ndege Mkoa wa Kigoma kuzingatia muda na viwango vya ubora ili kazi anazozifanya ziweze kuendana na kiwango cha Thamani halisi ya Fedha inayotolewa na Serikali.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo alipokutana na Ujumbe kutoka kwa Mkandarasi China Railway Engineering Group Company Ltd, ulipomtembelea ofisini kwake Manispaa ya Kigoma Ujiji kwa lengo la kutoa taarifa ya kuanza kwa kazi hizo.
Amesema uwanja huo utakapokamilika utaimarisha Sekta ya Biashara, Uchumi, Uwekezaji, Utalii na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa ndani na nje ya Mkoa wa Kigoma.
Aidha Andengenye amesema Serikali mkoani Kigoma itaendelea kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili iweze kufikia dhamira yake kwa lengo la kuleta mapinduzi katika Nyanja ya usafirishaji mkoni Kigoma na nchini kwa ujumla.
Meneja Kiwanja cha ndege Kigoma Mbura Daniel amesema kazi zinazofanywa na Mkandarasi huyo ni pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege Kigoma kutoka Mita 1,800 hadi 3,000 ujenzi wa jengo la Abiria, barabara za kuruka na kutua ndege.
Amezitaja kazi nyingine kuwa ni ujenzi wa eneo la maegesho ya ndege, jengo la zimamoto, mnara wa kuongozea ndege wakati wa usiku, uwekaji wa taa pamoja na barabara za kuingilia uwanja wa ndege, kazi inayotarajiwa kutekelezwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi Bil. 40.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa