MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE. DKT. PHILIP MPANGO AKIJIANDAA KUKATA UTEPE KUASHIRIA RASMI MAPOKEZI YA VIFAA TIBA KUTOKA TAASISI YA DORIS MOLLEL FOUNDATION NA WADAU WAKE OREXY GAS PAMOJA NA TUME YA USHINDANI (FCC) KWA HOSPITALI YA WILAYA BUHIGWE. WA KWANZA KULIA KWAKE NI DORIS MOLLEL, AKIFUATIWA NA MKUU WA MKOA WA KIGOMA MHE. THOBIAS ANDENGENYE.
MUASISI WA TAASISI ISIYO YA KISERIKALI YA DORIS MOLLEL FOUNDATION BI. DORIS MOLLEL AKIZUNGUMZA KWENYE HAFLA YA MAPOKEZI YA VIFAA TIBA VILIVYOTOLEWA NA TAASISI YAKE KWENYE HOSPITALI YA WILAYA YA BUHIGWE JULAI 6,2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake wajawazito umekuwa ukichangia kuzaliwa kwa watoto njiti katika Jamii.
Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo alipozungumza aliposhuhudia mapokezi ya vifaa Tiba pamoja na vitendea kazi kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Buhigwe mkoani hapa.
Amesema uwepo wa changamoto kama mimba za utotoni, msongo wa mawazo, vipigo, ukosefu wa lishe bora, pamoja na tabia nyingine zisizo za kiutu wanazotendewa wanawake wajawazito, kumechangia kusababisha baadhi yao kujifungua kabla ya wakati.
Amesisitiza kuwa, pamoja na uwepo wa sababu za Maradhi ya mfuko wa uzazi, mimba ya zaidi ya mtoto mmoja na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza, wanawake wengi wamekuwa wakipatwa na tatizo hilo kutokana na changamoto za kimaisha zinazosababishwa na watu wa karibu ndani ya jamii.
Aidha, Dkt Mpango ameishukuru Taasisi ya Doris Mollel ikishirikiana na wadauwake kwa kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye Thamani ya Shilingi Mil. 190 katika Hospitali ya Wilaya ya Bihigwe zikiwemo Mashine 16 za kupima mapigo ya moyo, vitanda saba vya kujifungulia, viwili vya kupimia na vitatu vya kulalia wagonjwa.
Pia Taasisi hiyo imetoa magodoro 17, mashuka kumi, mashine mbili za kuzalisha hewa safi, hadubini moja na mashine 11 za kupima wingi wa damu.
Aidha Dkt. Mpango ameshuhudia ugawaji wa mitungi 300 ya Gesi iliyotolewa na kampuni ya Orexy Gas ya nchini, ambapo majiko214 yametolewa kwa wanawake wajawazito na16 kwa wasaidizi wa Afya.
Pia Makamu wa Rais Dkt. Mpango ameshudia mapokezi ya madawati 450 yaliyotolewa na Tume ya Ushindani nchini.
Awali akiwasilisha Taarifa ya ufadhili wa vifaa Tiba kwenye Hospitali ya wilaya Buhigwe, mwanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation Doris Mollel, amesema taasisi yake ilianzishwa mwaka 2015 ikilenga kusaidia Serikali kupunguza vifo vya watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti).
Amesema katika kipindi cha miaka 8, Taasisi ya hiyo imechangia vifaa Tiba katika Hospitali 64 nchini vikiwa na Thamani ya zaidi ya Shilingi Bil. 1.2.
Mollel amesema ‘’tumefanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za nchi 11 Duniani, na kupitia utafiti huo taarifa iliyotolewa olibainisha kuwa kila baada ya sekunde 2 mtoto anayezaliwa kabla ya wakati anapoteza maisha’’
Ameendelea kusema kuwa, njia pekee ya kupunguza idadi ya vifo ni kutengeneza mazingira bora ya miundombinu ya kiafya kwa ajili ya kukabiliana na sababu za vifo hivyo pamoja na kuhakikisha jamii inaelimishwa ili iweze kutambua na kuchukua hatua dhidi ya changamoto hiyo.
Molle amewahimiza wadau wa maendeleo na wote wanaoguswa na dhamira ya Taasisi ya Doris Mollel Foundation kuendelea kuchangia kwa kutoa misaada mbalimbali kupitia Taasisi hiyo ili iweze kuendelea kuigusa jamii kupitia mpango wao wa kunusuru maisha ya watoto njiti nchini.
‘’Mojawapo ya njia tunazotumia kupata fedha ni kupitia Matamasha mbalimbali ya michezo na burudani tukishirikiana na wanamichezo na wasanii maarufu, ambapo kupitia majukwaa hayo tunapata wasaa wa kukutana na wadau wetukwa lengo la kutuchangia fedha tunazoendelea kuzitumia kwa ajili ya kununua vifaa tiba’’ amefafanua Mollel.
Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Buhigwe wameonyesha kuguswa na msaada huo huku wakiishukuru Taasisi ya Doris Mollel kwa kuwaletea mapinduzi ya kifikra kuhusu namna bora ya kuishi na kina mama wajawazito pamoja na kuepuka vitendo vinavyoweza kuwa visababishi vya uzazi wa watoto njiti.
Pia wanufaika waliopata ufadhili wa mitungi na majiko ya Gesi, wamesema msaada huo utawapunguzia adha ya kutumia muda mwingi kwa ajili ya kutafuta kuni.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa