Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2022 Sahili Geraruma amewataka Wataalam wa Serikali wenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo, kuzingatia Taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali katika utendaji kazi wao.
Geraruma aliyasema hayo wakati akizindua mradi wa vyumba sita vya Madarasa katika Shule ya Sekondari Nyanganga iliyopo wilayani Uvinza Mkoani hapa, ambapo Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge alimtaka Mhandisi anayesimamia ujenzi wa mradi huo kuzingatia michoro ya majengo inayotolewa na Serikali.
‘‘Nakushauri Mhandisi pamoja na wataalam wengine mnaosimamia kazi za ujenzi hapa, muache kukaa ofisini na badala yake mfike maeneo inakotekelezwa miradi ya Ujenzi ili kubaini na kuzifanyia kazi dosari zinazoweza kujitokeza wakati ujenzi ukiendelea’’ Alisema Geraruma.
Aidha kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge, alikubali kuzindua Mradi huo wenye Thamani ya Shilingi Milioni mia moja na Ishirini na kumuagiza Mhandisi wa Wilaya ya Uvinza kufanya marekebisho katika maeneo yenye dosari alizozibaini.
Kapitia hotuba yake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye alisema Mwenge huo utakimbizwa katika Halmashauri nane, ambapo utatembelea, kuweka mawe ya msingi pamoja na kuzindua jumla ya miradi 51 yenye Thamani ya zaidi ya Shilingi Bil.13
Alifafanua kuwa, Mkoa ulifanya vizuri katika zoezi la Sensa ya watu na Makazi kwa Mwaka 2022, pia umeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, Utekelezaji wa Afua za Lishe ili kukabiliana na Udumavu pamoja na Mapambano dhidi ya Malaria.
‘‘Nachukua fursa hii kuwapongeza wakimbiza Mwenge Kitaifa kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya kwani mpaka kufikia sasa wamefanikiwa kuifikia Mikoa 29 yenye Jumla ya Halmashauri 179 na kuifikisha alama ya chombo hiki kilichoasisiwa kwa nia ya kutuunganisha’’ Alisema Andengenye.
Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako, alisema ameridhishwa na mapokezi makubwa ya Mwenge yaliyofanyika wilayani Uvinza huku akisisitiza kuendelea kuutumia kwa kusambaza ujumbe wa kupinga rushwa, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kuhamasisha uzalendo.
‘‘Nawasihi tutumie Mwenge wa Uhuru kama chombo cha kujitafakari na kuchukua hatua pale tunapoona baadhi yetu wanakiuka maadili mema hali inayoweza kuharibu Amani na mshikamano uliopo katika Nchi yetu’’ alisisitiza Ndalichako.
MKOA WA KIGOMA
Anuani: S.L.P 125
Simu: 0282802330
Simu ya kiganjani: +255766853404
Barua Pepe: ras@kigoma.go.tz / ras.kigoma@tamisemi.go.tz / info@kigoma.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Kigoma. Haki zote zimehifadhiwa